Rais Samia akagua miradi ya maendeleo Tanga

By Hamida Kamchalla , Nipashe Jumapili
Published at 05:58 PM Feb 23 2025
Rais Samia akagua miradi ya maendeleo Tanga
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Samia akagua miradi ya maendeleo Tanga

Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ziara yake mkoani Tanga inalenga kukagua miradi ya maendeleo na kimkakati pamoja na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali baada ya serikali kuwekeza kiasi cha shilingi trilioni 3.6 katika maendeleo ya mkoa huo.

Akizungumza na wananchi leo katika Wilaya ya Handeni baada ya kuzindua hospitali ya wilaya hiyo, Rais Dk. Samia alieleza kuridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo, huku akibainisha kuwa licha ya kujengwa kwa hadhi ya wilaya, ina viwango vinavyostahili kuwa hospitali ya mkoa.

Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu shilingi bilioni 7, ambapo shilingi bilioni 3 zilitolewa na Serikali Kuu huku bilioni 4 zikitolewa na wahisani. "Nimepita kwenye hospitali ile na nimeelezwa kuwa ujenzi wake umekamilika. Kwa viwango ilivyojengwa, inastahili kuwa hospitali ya mkoa na siyo ya wilaya pekee," amesema Rais Dk. Samia.

Katika ziara yake mkoani Tanga, Rais anatarajiwa pia kutembelea Bandari ya Tanga, ambayo imeendelea kufanya vizuri baada ya serikali kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 429.1 katika maboresho makubwa ya miundombinu yake.