WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku akisisitiza kuwa wagombea wa urais wa chama hicho hawatakuwa na kazi kubwa kwakuwa wataingia kwenye uchaguzi wakiwa na rekodi thabiti ya utekelezaji wa ilani ya chama.
AkIzungumza katika mkutano wa CCM jimbo la Maswa mkoani Simiyu leo Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi chama hicho kitaendelea kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana.
Amesema suala hilo litafanyika ili wagombea wa chama hicho wasiwe na kazi kubwa ya kueleza waliyoyafanya, badala yake watumie muda wao kuomba kura.
“CCM ni chama kikubwa, pendwa na kinachoaminiwa, kina sera zinazotekelezeka, kikiahidi, kinatekeleza. Wanamaswa, leo mpo hapa na mbunge wa Maswa Mashariki, anawaeleza yanayotekelezwa ili mgombea wetu atakapofika hapa, kazi yake iwe ni ndogo ya kuomba kura,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amebainisha kuwa wakati wa kampeni, Mgombea Urais wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, watafika Maswa kuzungumza na wananchi na kueleza mipango yao kwa miaka mitano ijayo.
“Wakati wa kampeni, Rais Samia na mgombea mwenza wake Dk. Nchimbi watakuja Maswa kuomba ridhaa yenu. Tunataka kazi yao iwe nyepesi kwa sababu tayari mmeona kazi nzuri iliyotekelezwa,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa Rais Hussein Mwinyi, ambaye ni Mgombea Urais kwa upande wa Zanzibar, ataendelea na kampeni zake visiwani humo huku chama kikiendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha maendeleo yanafika kila kona ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED