Biteko asisitiza Watanzania kumuombea Rais Samia, nchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 04:59 PM Feb 16 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akifuatilia mafundisho
mbalimbali kutoka kwa wachungaji wa Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es
saalam leo Februari 16, 2025 aliposhiriki ibada ya jumapili
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akifuatilia mafundisho mbalimbali kutoka kwa wachungaji wa Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es saalam leo Februari 16, 2025 aliposhiriki ibada ya jumapili

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ametoa wito kwa Watanzania, kuendelea kuiombea nchi pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Tuendelee kuliombea kanisa, tuendelee kuiombea nchi yetu na Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa kweli anafanya kazi nzuri na sisi tunaofanya kazi karibu naye tunaona,” amesema Dk. Biteko.

Biteko amesema hayo leo, Februari 16, 2025 wakati akishiriki ibada katika Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe, Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Amewahimiza Watanzania kudumisha upendo na amani nyakati zote, hususan kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ili usiwe sababu ya kuligawa taifa kutokana na tofauti ya mitazamo.

“Mungu ametupa bahati ya kuwa na nchi yenye amani, sisi tuilinde kwa wivu mkubwa, kwa kuwa amani ikiondoka gharama yake ni kubwa. Tuziombee  pia nchi jirani zenye matatizo, kwa vile tatizo la jirani linaweza kuwa tatizo lako wakati wowote ule, mfano mnakumbuka janga la Uviko-19 lilivyotuathiri dunia.”

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa serikali imeendelea kuboresha mipango na sera mbalimbali,  ili kuendana na mahitaji ya dunia, ametolea mfano mabadiliko yaliyofanyika katika Sera ya Elimu.

 “Tunatengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo, ambayo tulizunguka nchi nzima, kwa ajili ya kukusanya maoni ya watu katika makundi mbalimbali, ili tuweze kupata Tanzania tunayoitaka miaka 25 ijayo,” amebainisha Dk. Biteko.

Akihuburi wakati wa ibada hiyo, Mchungaji Dk. Joseph Mayala Mitinje, amewaasa waumini wa kanisa hilok kukumbuka kufanya maombi na kusema ibada hiyo ilikuwa maalum, kwa ajili kuiombea serikali pamoja na mahitaji mbalimbali.

“Ili umtumie Mungu vizuri una mahitaji ya kila eneo, hivyo asubuhi ya leo tunaombea mahitaji yetu kwa Bwana,” amesema Dk. Mitinje.Aidha, amesema kwa kuliombea taifa pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali katika kutekeleza majukumu yao, huku akibariki Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani, umoja na mshikamano.

Mchungaji Andrew Chad, kutoka nchini Uingereza, akihubiri katika ibada hiyo, amesema makanisa ya Uingereza na Tanzania, yamekuwa na ushirikiano wa karibu na hivyo imeendelea kumpa fursa ya kuhubiri injili nchini.

Ameeleza alipokuja nchini alianza kuhubiri injili katika Kanisa la AICT Mpanda, mkoani Rukwa, kwa muda wa miaka minane na baadaye yeye na wenzake  walianzisha makanisa maeneo mbalimbali, ikiwamo mkoani Tanga, alihudumu kwa muda wa miaka sita.

 “Tulipata wito kwenda mkoani Tanga, kuhubiri injili, kwa upande wa watu wa kabila la Wadigo na kuwafundisha watu, wanampenda Mungu,” amesema Mchungaji Chad.