WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema itaendelea kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini, na kuwafikia wote wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati, kwa shule za sekondari nchini.
Mafunzo hayo yanahusisha mbinu mbalimbali za ufundishaji, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), kwa lengo la kuboresha ufundishaji na kuongeza ufanisi katika masomo hayo.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Sera, Utafiti na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Emmanuel Kilundo, ameyasema hayo, alipotembelea kituo cha mafunzo, kwa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara yakiwahusisha walimu kutoka mikoa ya Njombe, Lindi na Mtwara.
Amesema mafunzo hayo endelevu, yatasaidia walimu kuboresha ufanisi wao kazini na kutumia teknolojia katika ufundishaji, jambo ambalo linatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu hususan masomo ya sayansi na hisabati.
Kuhusu utekelezaji wa mafunzo hayo, Kilundo amesema kuwa wanawajengea uwezo wathibiti ubora wa shule, ambao watasaidia kusimamia mifumo ya ufuatiliaji, ili kuhakikisha kuwa mbinu zinazotolewa zinatekelezwa ipasavyo shuleni.
“Wathibiti ubora, baada ya kupata mafunzo maalum, watafuatilia utekelezaji wa mbinu hizo kwa karibu, kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu inayozingatia viwango vya ubora,” amesema Kilundo.
Ameongeza kuwa mbinu nyingine ya upimaji wa mafunzo hayo, ni kupitia mitihani inayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), matokeo yatasaidia kupima kiwango cha uelewa na ufaulu kwa wanafunzi.
Ameongeza kuwa serikali imeanza kutekeleza Sera mpya ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na mitaala iliyoboreshwa, ambao unalenga kushughulikia changamoto kwenye masomo ya sayansi na hisabati.Anasema miongoni mwaka ni ukosefu wa mbinu za kisasa za ufundishaji, upungufu wa vifaa vya kufundishia kama maabara, matumizi duni ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), na ukosefu wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini (MEWAKA).
Amesema mtaala ulioboreshwa, unalenga kumjengea uwezo mwanafunzi kutumia maarifa, stadi na mitazamo chanya katika maisha ya kila siku.
“Mafunzo haya yanatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu nchini, wanafunzi wengi watahamasika kusoma masomo haya, kwa sababu yatafundishwa kwa mbinu rahisi na nyepesi, hivyo kushawishi wanafunzi kuyapenda.”
Mwenyekiti wa Wawezeshaji katika Mafunzo ya Walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati, ambayo yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Idara ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia (STEM), Dk. Absalom Mbiling’i, amesema kuwa hadi sasa kila mwalimu nchini amewezeshwa kufundisha angalau somo moja la sayansi.
Dk. Mbiling’i amesema kuwa kiwango hicho kikubwa kilichofikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha mchakato wa ufundishaji wa masomo ya sayansi.
Ameongeza kuwa, mafanikio hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma sayansi, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuandaa wataalam wengi ambao watasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii na watakuwa na uwezo kushindana katika fursa za kitaifa na kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED