JK asisitiza mabadiliko makubwa kiutendaji mageuzi kilimo Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:54 AM Feb 16 2025
Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete
PICHA:MTANDAO
Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete

Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, amesema Afrika inahitaji mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa kinachotegemea umwagiliaji, mbegu zinazohimili ukame na mabadiliko ya tabianchi.

Pia amesema zinahitajika mbolea bora na pembejeo za kisasa na kuongeza idadi ya mabwawa shamba ili kuwasaidia wakulima kuachana na kilimo cha mazoea.

Dk. Kikwete alisema hayo juzi alipoungana na viongozi mbalimbali wa Afrika katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika juzi jijini hapa. 

  Kuhusu uzalishaji duni wa Chakula katika Afrika, Dk. Kikwete alitaja changamoto zingine zinazokwamisha maendeleo ya kilimo kuwa ni ukosefu wa mikopo kwa wakulima, masoko ya uhakika na kiwango kidogo cha usindikaji wa mazao.

 Alisisitiza kuwa serikali peke yake haiwezi kutatua matatizo haya bali inahitaji kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula unakuwa endelevu.

 Akitoa mfano wa mafanikio ya Tanzania, Kikwete alitaja mradi kama wa Ushoroba (corridor) wa Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na Jenga Kesho iliyo Bora kupitia Kilimo (BBT), ambazo zinalenga kuimarisha sekta ya kilimo nchini.

 Katika mkutano huo, viongozi hao walijadili changamoto zinazoikumba sekta ya kilimo barani Afrika ambayo asilimia 80 ya watu wa bara hili wanaitegemea kwa chakula na kipato.

 Washiriki wengine wa kongamano hilo walikuwa Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan; Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger, Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.

 Katika mjadala ulioongozwa Desalegn, viongozi hao walibainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yameathiri sekta ya kilimo huku ukame, mafuriko, vimbunga na mvua isiyotabirika vikisababisha kushuka kwa uzalishaji wa chakula. Walisema hali hiyo inazidi kuhatarisha usalama wa chakula barani Afrika.

 Akifungua kongamano hilo, Rais wa Ethiopia, Taye Atske Selassie, alieleza jinsi nchi yake ilivyojitegemea kwa asilimia 100 katika uzalishaji wa ngano kutokana na mipango madhubuti ya kilimo cha umwagiliaji.

 Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya nchi za Afrika ni muhimu ili kubadilishana uzoefu wa kuboresha uzalishaji wa chakula.

 Katika kipindi hiki ambacho mataifa yaliyoendelea yamepunguza misaada  kwa Afrika, viongozi hao walikubaliana kuwa Afrika haina budi kuwekeza katika teknolojia za kilimo na miradi ya uzalishaji wa chakula kwa njia endelevu.

 Kwa  kutambua umuhimu wa mijadala kama hii, kongamano hili linatarajiwa kufanyika kila mwaka ili kuimarisha mshikamano wa Afrika katika kupambana na changamoto za tabianchi na usalama wa chakula.