MKUU wa wilaya ya Rorya mkoani Mara, Khalfan Haule, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya hiyo, Abdul Mtaka, kutekeleza kwa vitendo sera ya kuinua uchumi wa wananchi kupitia kilimo bora chenye tija.
Agizo hilo linakuja wakati wilaya hiyo ikiwa imepitisha makadirio ya matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 43, kutekeleza miradi ya maendeleo na matumizi mengine kama vile mishahara mwaka 2025/2026.
Kiongozi huyo aliwaambia wajumbe wa kamati ya ushauri(DCC) ya wilaya hiyo, mwishoni mwa wiki, kwamba watumie nafasi zao kuhakikisha wanasimamia mipango madhubuti ya kuwainua wananchi ambao wengi wanajishughulisha na kilimo.
"Lazima Mkurugenzi asimamie miradi ya kuboresha wakulima, kama vile utoaji wa pembejeo kwa wakati na kuhakikisha watumishi wa idara ya kilimo, wanatoa ushauri bora kwa wananchi, ili kupata mavuno bora,” alisema.
Aliwataka wakuu wote wa idara za halmashauri, kufanya kazi kwa bidii na kutoa elimu kwa wakulima na wajasiriamali ambao ni kundi kubwa katika jamii, ili kuinua uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED