MKUTANO wa viongozi wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Mashirika na Kampuni nchini (CEO- Roundtable) umeisifu serikali katika jitihada za ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kujenga uchumi kupitia sekta mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kwanza wa mwaka huu wenye ujumbe wa ‘Kutenga Jukwa kwa Uchumi Endelevu’ uliofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt-Roundtable, Santina Benson, alisisitiza kuwa umoja huo unashirikiana kwa karibu na serikali kuhakikisha sekta binafsi inashiriki katika sekta mbalimbali za uchumi, ili kuifanya Tanzania kuwa nchi isiyo tegemezi na kuendesha uchumi wake kupitia viwanda na biashara.
“Ndiyo maana CEOrt imekuwa ikifanya midahalo ili kuwezesha majadiliano juu ya masuala muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika kutimiza ndoto za Dira ya Maendeleo ya kutoka mwaka 2025 hadi 2050.
“Tunaishukuru serikali kwa jitihada zake za kubadilisha uchumi lakini tunahimiza kuzingatia maeneo muhimu yatakayotoa motisha kwa sekta binafsi kuchukua nafasi kubwa zaidi katika safari hii,” alisema.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Benson alisema CEOrt hivi karibuni ilizindua mradi wa kuwawezesha wanawake wa wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kiuchumi.
Mradi huo, kwa mujibu wa Benson, unasaidia wanawake wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha mapato yao na kukuza uhuru wao wa kiuchumi.
Prof. Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliiomba serikali kuzingatia ukuaji wa uchumi kama msingi wa maendeleo endelevu.
Alisema nchi imepitia mabadiliko magumu ya kiuchumi kuanzia kwa Rais mwasisi Mwalimu Julius Nyerere hadi viongozi waliomfuata, lakini katika kipindi cha hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikishuhudia ukuaji mzuri wa uchumi.
Aliongeza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2007, ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 11.9 na uliendelea kukua na kufikia asilimia 7.7 mwaka 2011.
Amesema ukuaji huo unatarajiwa kukua na kufikia kati ya asilimia 5.4 hadi 5.7 kwa mwaka huu.
Alitoa wito wa mapitio ya mfumo wa kodi ili uwe rahisi na kuvutia kwa wananchi kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi, ingawa alisema kuwa bado kuna kuna changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma maendeleo ikiwemo rushwa.
Prof. Kinyondo alisisitiza kwamba juhudi za serikali za kubadilisha uchumi zinapaswa kuhusisha sekta binafsi kwa kutumia rasilimali zilizopo. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti ili kupata majibu ya changamoto katika sekta mbalimbali nchini.
“Mara nyingi tunategemea wahisani kufadhili utafiti mbalimbali na baadhi yao huja na masharti yao. Nadhani ni wakati wa serikali kuanza kufadhili utafiti katika maeneo kama kilimo ili kuleta tija zaidi kwa nchi,” alisema.
Akichangia hoja katika mjadala huo, Dk. Donald Mmari kutoka Programu ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA), alielezea umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na jamii katika kutumia rasilimali zilizopo kujiletea maendeleo kupitia sekta mbalimbali za kimkakati kama vile teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), madini na utalii ili kuendesha uchumi.
“Tuna rasilimali nyingi ambazo hazijatumiwa ipasavyo ambazo zinaweza kuchukua jukumu kubwa katika ukuaji wa Uchumi. Awali, tulikuwa na mikakati kama vile Mkakati wa Taifa wa Ukuaji na Kupunguza Umaskini (Mkukuta) katika kupambana na umaskini.
“hivi karibuni, tulikuwa na nafasi kubwa kutokana na uwapo wa maendeleo ya kiteknolojia, ambayo inatuwezesha kutumia rasilimali hizi kuvutia biashara zaidi na kufikia malengo yetu ya 2050,” alisisitiza.
CEO Rountable inajumuisha wakurugenzi na watendaji wakuu kutoka zaidi ya kampuni 200 wa sekta mbalimbali nchini. Wanachama wake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi kwa kuchangia kodi na mchango mkubwa wa ukuaji wa sekta binafsi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED