Halmashauri Ushetu yaja na 'dawa' ya ufaulu

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 05:00 PM Feb 23 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akizungumza na walimu 1,228 wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Ushetu (hawapo pichani), wakati wa kikao kazi cha tathimini ya Kutokomeza Zero, kilichofanyika juzi, Kata ya Nyamilangano.
Picha: Shaban Njia
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akizungumza na walimu 1,228 wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Ushetu (hawapo pichani), wakati wa kikao kazi cha tathimini ya Kutokomeza Zero, kilichofanyika juzi, Kata ya Nyamilangano.

HALMASHAURI ya Ushetu mkoani Shinyanga, imebuni mbinu mpya ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kwa kutoa motisha na vyeti vya pongezi kwa walimu wa masomo na shule zinazofanya vema kwenye mitihani ya mwisho.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ndiye aliyekabidhi vyeti vya pongeza na fedha taslimu, kwa walimu waliofanya vema kwenye masomo kutoka shule 10 bora wakati kikao cha tathimini ya elimu ya msingi na sekondari kilichofanyika Kata ya Nyamilangono na jumla ya walimu 1,228 walihudhuria.

Amesema vyeti hivyo, vikaongezee morari ya kufundisha, ili kuhakikisha wanaondoa sifuri katika mitihani ya darasa la nne na kidato cha tano, kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanakatishwa tamaa ya uwapo wa kazi shuleni zisizoendana na umri wao.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akimpatia cheti cha pongezi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Songambele, Maria Thomas, kwa kufaulisha wanafunzi wote katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2024.
Macha amesema, bado kuna tatizo la mimba na ndoa za utotoni  kwa wanafunzi pamoja na kutokumaliza elimu ya msingi hasa wa kike ukilinganisha na wa kiume na kuwataka viongozi wa serikali za vijiji na kata kuyasimamia hayo yasiendelee kujitokeza.

Amewataka walimu kutokukata tamaa ya kupambana na utoro, kwa wanafunzi na badala yake wawahamasishe wanafunzi wapende masomo, ili kama kuna mzazi atabainika kumshawisha mtoto kuolewa au kuchunga mifugo wataweza kupata taarifa na kuchukua hatua za haraka.

Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi, Zelena Ntulo, amesema vyeti vya pongezi na fedha vinataolewa kwa Mshindi wa Taalumu Shuleni, kwa shule 10 bora, Mabingwa wa Somo kwa kila somo, shule zilizoongeza ufaulu na Usimamizi Bora wa Miradi ya Shule kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha na ubora wa majengo.

Walimu wa shule za msingi na sekondari Halmashauri ya Ushetu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (hayupo pichani).
Ntulo amesema, zaid#i ya Sh. milioni tano zimetolewa kwa walimu hao na utaratibu huo waliuanzisha tangu mwaka 2023/2024 na umesaidia kuweka ushindani wa shule katika kufaulisha masomo ya sayansi na biashara na mwakani pia watakawapatia vyeti vya pongezi na fedha.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hadija Kabojela, amesema utaratibu huo waliona ni njia ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hasa wa kike ambao wamekuwa wakikatisha masomo, kwa sababu mbalimbali ikiwamo utaro.

Amesema, tathimini waliyofanya kabla ya kutoa vema itaongeza ufaulu kwa wanafunzi na kupunguza ufaulu wa wastani wa divisheni nne na sifuri, kwa kuwa miaka ya nyuma walikuwa na sifuri 300 katika shule za msingi na sekondari na sasa zimebaki 47 ambazo nazo wanapambana kuziondoa.