EU kutathmini mradi wa Global Gateway

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:22 PM Feb 23 2025
EU kutathmini mradi wa Global Gateway
Picha: Mpigapicha Wetu
EU kutathmini mradi wa Global Gateway

WABUNGE saba wa Bunge la Ulaya (MEPs), kutoka Kamati ya Maendeleo watafanya ziara nchini Tanzania kuanzia Februari 24 hadi 26, mwaka huu.

Lengo ni kutathmini athari za uwekezaji wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na ufanisi wa mkakati wa Global Gateway, unaosaidia miradi ya miundombinu na maendeleo duniani kote.

Ujumbe huo, unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo, Barry Andrews, na utatembelea miradi inayohusiana na maji na usafi wa mazingira, maendeleo ya uchumi na miundombinu ya bandari, usawa wa kijinsia, elimu na uvuvi endelevu. 

Kamati hiyo ya Maendeleo inasimamia sera za misaada ya maendeleo na ushirikiano wa EU. Ziara hii ya ukaguzi itawawezesha wajumbe kutathmini jinsi fedha za EU zinavyotumika katika miradi halisi nchini.

Wabunge hawa wa Ulaya watakutana na Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk. Tulia Ackson; Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo; na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi.

Aidha, watafanya mazungumzo na wawakilishi wa ujumbe wa kidiplomasia wa EU, mashirika ya Umoja wa Mataifa, benki za maendeleo, sekta binafsi, mashirika ya kitaifa ya maendeleo, na asasi za kiraia za ndani.

Miongoni mwa masuala watakayojadili ni maendeleo endelevu, ushirikiano wa mabunge, na haki za binadamu.

Kuhusu Kamati ya Maendeleo (DEVE), Kamati ya Maendeleo ya Bunge la Ulaya inahusika na kuunda sera za maendeleo ya kimataifa na misaada ya kibinadamu. Inasimamia miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na EU kote duniani, kuhakikisha inaendana na malengo ya maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimataifa.

Wajumbe wa Ujumbe wa Bunge la Ulaya; Barry ANDREWS – Mwenyekiti wa DEVE, Renew Europe (Ireland); Lukas MANDL – European People’s Party (Austria); Niels GEUKING – European People’s Party (Germany)

Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdau muhimu katika ushirikiano na Tanzania pamoja na Afrika Mashariki. Umoja wa Ulaya imeanzisha mkakati wa Global Gateway ili kukuza nadhifu, usafi na usalama wa kijitali, sekta za nishati na usafiri pamoja na kuimarisha afya, elimu na mfumo wa utafiti duniani kote. 

Mkakati wa Global Gateway unatekelezwa kwa pamoja chini ya timu ya nchi za Ulaya, ambazo ni taasisi za Umoja wa Ulaya na Nchi Wanachama wake.