MazaoHub yashinda tuzo kampuni bora ya teknolojia katika kilimo

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 04:35 PM Feb 23 2025
Baadhi ya maofisa wa Kampuni ya MazaoHub wakishangilia baada ya kutwaa tuzo hiyo.
PICHA:MPIGAPICHA WETU
Baadhi ya maofisa wa Kampuni ya MazaoHub wakishangilia baada ya kutwaa tuzo hiyo.

KAMPUNI ya MazaoHub imeshinda tuzo ya kampuni bora inayojihusisha na teknolojia kwenye kilimo, katika mashindano ya Africa Best Tech yaliyofanyika nchini Uganda hivi karibuni.

Kampuni hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi wake Geophrey Tenganamba, imejikita kwenye matumizi ya teknolojia kwa wakulima, na inafanya kazi katika mikoa 15 nchini ambayo ni Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe, Morogoro, Rukwa, Pwani na Mtwara.

Mikoa mingine ni Kigoma, Katavi, Kagera, Tabora, Manyara, Tanga, na Singida, inashirikiana na Maafisa Ugani wa Serikali kupitia Farmer Excellence Centers.

 MazaoHub ni zao la Programu ya Jenga Kesho Bora kwa upande wa Teknolojia (BBT- Technology).

 Programu hiyo, inatumia njia za kisasa za upimaji wa udongo pamoja na kuwafikia wakulima nchini kwa matumizi sahihi ya Teknolojia ya Mawasiliano ikitumia kituo chake cha huduma kwa wateja kinachofanya kazi kwa njia ya simu.

 Akizungumzia ushindi huo Tenganamba ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Kilimo akisifu imekuwa msaada mkubwa wa mafanikio katika kampuni yake.

 "Kampuni hii tangu ilipoanza imekuwa inashikwa mkono na Wizara ya Kilimo, kwa kuunganishwa na wadau katika sekta ya kilimo hasa kupatiwa nafasi katika maonesho makubwa ya ndani na nje ya nchi, hatua hii imeiwezesha kampuni kujulikana na kusaidiwa kwa namna mbalimbali." amesema 

 Amesisitiza kuwa MazaoHub inajenga mahusiano imara na wakulima kupitia Mbinu ya 'Rolodex' inayotumika kuhakikisha kila mkulima anapata huduma bora kwa kuwafuatilia kuanzia upandaji hadi mavuno na masoko.

 "Chini ya Mfumo huo MazaoHub hupata hadi taarifa binafsi za mkulima hatua inasaidia utoaji wa msaada wa kina zaidi."