WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Leila Mohammed Mussa, amewataka wanawake wajasiriamali kisiwani Pemba, kufanya kazi zao kwa kujiamini huku wakiwa na ubunifu na kuzalisha bidhaa zenye ubora, ili kuliendea soko la Afrika.
Leila ametoa wito huo katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake Chake, wakĂ ti alipokuwa akifungua kongamano la kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huashimiahwa kila mwaka ifikapo tarehe Machi 8.
Mwaka huu kwa upande wa taasisi ya Tanzania Women Chemba ya Biashara (TWCC), wameamua kuadhimisha siku hiyo kabla, kutokana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Amesema lazima mjasiriamali awe na nidhamu na kile anachokifanya huku akiwa mwangalifu pamoja na kujali wakĂ ti, ili kupata manufaa makubwa kupitia kazi zake.
Aidha amewataka wajasiriamali hao kutumia fursa iliopo kufanyakazi, kwa bidii huku wakiwa wabunifu na kuleta tofauti kubwa ya bidhaa zao, ili kukabiliana na ushindani wa kibiashara.
Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Mgeni Khatib Yahya, amewataka wanawake kutumia fursa iliyopo katika mitandao ya kijamii Kwa kutangaza biashara zao.
"Mitandao ya kijamii ni fursa nzuri ya kutangaza biashara zako, lakini mara nyingi watu hutumia kutangaza mambo yasio faa na kuipoteza nafasi hiyo," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Katika hatua nyengine, Mkuu huyo wa Wilaya, amewataka wanawake hao mbali ya shughuli zao za ujasiriamali kuwa tayari kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, ili waweze kusaidia kutatua changamo to mbali mbali zinazowahusu wanawake.
"Shida za wanawake wanaozijua ni wanawake wenyewe hivyo wakipata fursa ya kuingia katika nafasi za maamuzi itakuwa rahisi kusaidia kuondoa changamoto hizo," alisema Mgeni,
Mkurugenzi Mtendaji TWCC, Mwajuma Hamza alisema bado wanawake wamekuwa wakifanya biashara ndogo ndogo, lakini kupitia taasisi hiyo, watahakikisha wanawawezesha wanawake, kwa lengo la kupiga hatua kubwa kibiashara na kuwa wajasiriamali wakubwa na kuweza kujitegemea
"Tumeweza kutoa mafunzo mbali mbali ya ujasiriamali Kwa wanawake wanachama kupitia taasisi hio hivyo ninaimani wanachama wetu wataweza kukuza kibiashara," alisema Mkurugenzi mtendaji huyo.
Akitoa ushuhuda juu ya namna walivyoahikwa mkono na TWCC, Hindu Khamis Ali, kutoka Wete Pemba, amesema kutokana na mafunzo aliyoyapata kupitia taasisi hiyo, sasa kwa kiasi kikubwa ameweza kujikwamua kiuchumi.
"Naweza kusarifu bidhaa zangu pamoja na kuweka katika vifungashio vizuri hivyo najivuania mafunzo hayo," alisema Hindu.
Shuwayla Ali kutoka Vitongoji Chake Chake, alisema atakuwa mwizi wa fadhila iwapo hataishukuru TWCC, kwa namna walivyomwezesha katika shughuli hizo za ujasiriamali na sasa kuwa mjasiriamali anayetambulika
"Sikutarajia kama Kuna siku nitatoka katika nje ya Kisiwa cha Pemba kwa shughuli hizi za ujasiriamali lakini kupitia TWCC nimeweza," alisema Shuwayla.
Aidha Nassra Nassor Omar wa Kiuyu, alisema kutokana na juhudi za TWCC katika kuwainua wanawake hivi sasa wanawake wengi ni wajasiriamali, jambalo ambalo limewafanya kuondokana na utengemezi na kuanza kujitegemea wenyewe.
"Hivi sasa miongoni mwetu wameshavuuka kutoka wajasiriamali wadogo na kuwa wakubwa kupitia nguvu ya TWCC," alisema Nassra.
Hata hivyo wajasiriamali hao wameiomba TWCC kuendelea kuwashika mkono, hadi kuhakikisha wanapiga hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo na kupata mafanikio makubwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED