Wengi wape lakini wachache wasikilizwe

By Ida Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 07:58 AM Jan 22 2024
Mahakamani
PICHA: MTANDAONI
Mahakamani

MADA ya leo ni kuhusu Haki, Haki, Haki! Ya wengi wape lakini wachache pia wasikilizwe. Katiba ndiyo sheria mama inayotoa haki zote za watu wote wa Tanzania.

Hili ni ombi kwa jicho  na sikio la Rais Samia Suluhu Hassan kuziangazia haki tatu kuu kwenye katiba yetu ambazo zimeporwa na serikali zilizotangulia.  Serikali, Bunge, Mahakama, hazina uwezo wala mamlaka ya kupora haki yoyote iliyotolewa kwa mujibu wa Katiba kwa sababu katiba iko juu na mihimili hiyo yote mitatu iko chini ya Katiba.

 Mihimili miwili, Serikali na Bunge imepoka haki ya Mtanzania kuchagua na kuchaguliwa zilizotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) ya mwaka 1977. Serikali na Bunge zilipata wapi uwezo na mamlaka ya kuzipora haki hizi? Mpaka  ninapoandika hapa, haki hizi bado zimeporwa. Mtanzania hana haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka kwa sababu haki ya kila Mtanzania kugombea imepokwa na kikundi kidogo cha watu wanaoitwa chama cha siasa. 

 Chama cha siasa ndicho kimepewa mamlaka ya kuamua nani agombee na si wagombea au wananchi, matokeo yake wananchi wanalazimishwa kuchagua viongozi walioletewa na vyama vya siasa kitu ambacho si sahihi kabisa, si haki na ni dhambi. Usikute  ndiyo sababu karma kila siku inawatafuna viongozi wetu.

 Rais Samia, analiishi jina lake la Suluhu kwa kauli na matendo kwa kuleta suluhu ya kweli ya mtanziko wa kisiasa unaolikabili taifa letu.  Ameonyesha kwa kauli na matendo anataka maridhiano ya kweli ndiyo maana amekubali kubadili sheria mbalimbali. Mabadiliko haya ni fursa ya kuzirejesha haki za msingi za Watanzania zilizoporwa. Kwa vile aliyezipora haki hizo si yeye bali kaingia na kukuta zimeishaporwa na sasa anafanya marekebisho tu ya sheria, lakini zile haki porwa za katiba  haziguswi? 

 HAKI KUU ZA MTANZANIA 

Haki ziko nyingi, lakini nitajikita kwenye haki tatu kuu za Mtanzania. Haki kuu ya kwanza ni ya uraia. Mtu yoyote akizaliwa ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakuwa raia wa Mtanzania kwa kuzaliwa.  Haki  hii ni haki ya kwanza ya msingi ambayo ni  ya kuwa Mtanzania. Haki hii haiwezi kuondolewa na mamlaka yoyote, ila mtu anaweza kuipoteza endapo ataukana uraia wako. 

 Kwa maniki hiyo, ile sheria yetu ya kuwa mtu akichukua uraia wa nchi nyingine yoyote, anaupoteza utanzania wake, ni batili na ni kinyume cha katiba. Hata hivyo, ubatili huu, haujabatilishwa kwasababu hakuna aliyefungua shauri mahakamani kuipinga.

 Haki kuu ya pili ni ya kuchagua iliyotolewa na ibara ya Tano  ya Katiba ya JMT. Haki hii ni kila raia wa Tanzania anapofikisha umri wa miaka 18, ana haki ya kuchagua kiongozi wake. Haki hii inatekelezwa kwa kila mtu kujiandikisha kupiga kura na haiwezi kuondolewa na mamlaka yoyote. 

Kwa Tanzania, haki hii imefinyangwa finyangwa kwa baadhi ya watu kunyamaza kwa kufungwa gerezani, wagonjwa hospitalini na Watanzania walioko nje ya nchi. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, uandikishaji unaotumia BVR hivyo kwa kutumia ‘biometric data’, kitambulisho cha taifa au passport ambavyo vyote vina ‘biometric data’, vinaweza kutumika kuwawezesha Watanzania wote popote walipo kumchagua Rais wa Tanzania na wa Zanzibar.

Haki kuu ya tatu ni ya kuchaguliwa kupitia ibara ya 21 ya Katiba ya JMT. Kwa  mtu mwenye umri wa miaka 21, yuko huru kugombea nafasi yoyote ya uongozi kuanzia serikali za mitaa hadi serikali kuu. Haki hii ni ya msingi na haiwezi kuondolewa na mamlaka yoyote. 

Hata hivyo, kwa Tanzania, haki hii ya kila Mtanzania ana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi na kuchaguliwa imefutwa kwa kuchomekewa sharti la kudhaminiwa na chama cha siasa. Sharti hili ni batili.

HITIMISHO

Waungwana wanapotaka jambo lao kubwa, wakakaa pamoja kukubaliana na kukuta wamepewa kidogo  ya kile walichotarajia, hawaziri, hawasusi wala kutaka kupeleka watu barabarani. Waungwana hupokea kidogo walichopata na kuendelea kuomba kikubwa.

 Kwa vile matatizo makubwa ya siasa zetu yako kwenye Katiba, tulianza mfumo wa vyama vingi kwa katiba ya chama kimoja.  Ili kuwatendea haki Watanzania,  tunaendelea kumwomba kwa unyenyekevu Rais Samia aendelee kuliishi jina lake kwa kuleta suluhu ya kweli ya mtanziko wa siasa zetu. 

 Kwa mambo makubwa na mazuri anayoyafanya, Watanzania wengi wanamkubali.  Lakini  maoni ya wachache wanaotaka tufanye kwanza mabadiliko madogo ya katiba,  pia yasikilizwe ili tufanye mabadiliko ya sheria ziwe za haki kwa wote. Wengi  wape, wachache pia wasikilizwe.

 

Mungu Mbariki Rais Samia

Mungu Ibariki Tanzania.

 

Paskali 

0754 270403