Bodaboda waanza mwaka kwa kukabidhiwa helmet 200

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:28 PM Jan 05 2025
Usafiri wa bodaboda ni maarufu maeneo ya mijini na vijijini
Picha: Mtandao
Usafiri wa bodaboda ni maarufu maeneo ya mijini na vijijini

WAENDESHA pikipiki wa kata ya Mbwara, Mkoa wa Kipolisi Rufiji wamepatiwa kofia ngumu (helmet) kwa ajili ya kutumia wakiwa kwenye shughuli zao za usafirishaji.

Ugawaji kofia ngumu hizo ulifanyika Desemba 31 mwaka jana, ukiongozwa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahimu katika hafla iliyoratibiwa na Mkaguzi Kata wa Kata ya Mbwara, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Faustina Ndunguru na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Miongoni mwa waliohudhuria ni Diwani wa Kata hiyo, Juma Ligomba pamoja na wananchi na viongozi wengine wa Jeshi la Polisi, huku mgeni rasmi akiwa ni Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, ACP Grafton Mushi.

Kwa kutambua nafasi ya bodaboda katika kusafirisha abiria, Jeshi la Polisi lilitumia nafasi hiyo kutoa elimu ya usalama  barabarani sambamba na elimu ya ushirikishwaji jamii katika kuzuia makosa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji watoto.

Kata ya Mbwara yenye vijiji vitano, ina wakazi wenye mwamko mkubwa kuhusu uimarishwaji usalama, ikiwamo kufichua uhalifu na wahalifu kutokana na elimu ya mara kwa mara wanayopata kutoka kwa Mkaguzi Kata wa Kata hiyo ya Mbwara ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Faustina Ndunguru.

Mkaguzi huyo Msaidizi wa Polisi amekuwa anaendelea kujenga uhusiano na ushirikiano na wakazi wa vijiji hivyo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujitambua na kutambua nafasi yao katika kuimarisha ulinzi kwenye jamii yao.

Akizungumzia utoaji helmet hizo kwa bodaboda pamoja na elimu ya usalama barabarani, mkaguzi huyo alisema kuwa kwa muda mrefu bodaboda wamekuwa wakifundishwa masuala kadhaa ya usalama barabarani hususan kuepuka kuendesha kwa mwendokasi pamoja na uchukuaji tahadhari.

Alisema: "Leo hii viongozi wa Jeshi la Polis hapa Rufiji wamefika katika kata hii kukabidhi helmet hizi kwa bodaboda ikiwa ni mwendelezo wa elimu ya usalama barabarani na hasa kama inavyofahamika kuwa helmet ni kitu muhimu kwa bodaboda na abiria wao.

"Hivi karibuni ilitokea ajali ya bodaboda katika kijiji cha Nyamwage ambako bodaboda na abiria wake hawakuvaa helmet na wote walifariki dunia, tukio nililonilazimu kutafuta wadau wa kutoa helmet kwa ajili ya bodaboda ndipo nikaipata kampuni ya... (anataja jina la kampuni|) ikatupa helmet hizi.

Akizungumzia msaada huo kwa niaba ya bodaboda wengine, Katibu wa Bodaboda wa Kata hiyo, Fadhili Liato alipongeza Jeshi la Polisi, akiwamo mkaguzi wa kata hiyo kwa namna anavyoendelea kuwajengea uwezo katika kutambua umuhimu wa kushirikiana katika kudhibiti uhalifu sambamba na makosa ya usalama barabarani.