Vijana wachangia damu hospitali ya wilaya

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:35 PM Jan 05 2025
Uchangiaji damu huuokoa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, mama na mtoto
Picha: Mtandao
Uchangiaji damu huuokoa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, mama na mtoto

VIJANA 20 kutoka kikundi cha Mishemishe, kijijini Mangubu, kata ya Tongwe, wilayani Muheza, mkoani Tanga wamechangia chupa 11 za damu kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Muheza.

Uchangiaji huo uliofanyika hospitalini hapo umeongozwa na Diwani wa Tongwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza, Erasto Mhina na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Fani Mussa.

Akizungumza jana, Dk. Mussa aliwapongeza vijana hao kwa kuchangia chupa 11 za damu na kuwataka wawe mabalozi kwa wananchi wengine.

“Uchangiaji wa damu salama ni hiari na ni muhimu kwa sababu katika hospitali yetu tunauhitaji wa damu ili kuokoa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, ikiwa huduma za mama na mtoto zinaendelea, uhitaji wa damu salama ni mkubwa,” alisema Mussa.

Alisema wilaya ya Muheza imewekewa malengo na serikali kuchangia damu chupa 1,430 na hadi sasa wamevuka lengo kwa kukusanya chupa 1,694 sawa na asilimia 118.5.

Meneja wa huduma za maabara hospitali hiyo, Doreen Owen, alitoa elimu ya uchangiaji wa damu kwa vijana hao kupima uzito, shinikizo la damu na wingi wa damu.

Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Wilaya ya Muheza, Mohamed Zuberi Mzee, alitoa rai kwa wananchi wote kujitokeza kuchangia damu salama ambayo itasaidia kuokoa uhai wa wagonjwa.

Awali, Mhina alisema kujitolea kuchangia damu ni jambo la baraka kwa kuwa linawasaidia wagonjwa wa ajali, wajawazito na watoto.

Alisema hospitali hiyo iko pembezoni mwa barabara kubwa, hivyo inapokea majeruhi pindi ajali inapotokea na kwamba hilo ndilo lililowasukuma kuchangia damu.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Mishemishe, Peter Mwandege, alisema wanachama wake ni wajasiriamali na kwamba wamechangia damu ili wawe sehemu ya kuokoa vifo kwa wagonjwa wanaohitaji damu.

Kaulimbiu ya uchagiaji huo ni 'Changia Damu Usichangie Msiba'.