WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amekiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuwaangalia wawekezaji wazawa kwa jicho la pekee, huku Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), akiwaagiza kudhibiti bidhaa feki.
Mkumbo ametoa agizo hilo leo, Mjini Babati, mara baada ya kutembelea kiwanda cha Mati Super Brands Limited, kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa, David Mulokozi.
"TIC wawekezaji kama hawa muwape jicho la pekee kila wanachohitaji wapewe, ili waweze kufanya uwekezaji wao," amesema Mkumbo
Prof. Mkumbo amesema uwekezaji unaofanywa unasaidiwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati ( BAWASA), ambao ndio watoa huduma ya maji.
Aidha amesema suala la bidhaa feki lililoelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited, Mulokozi wanalichukua kwa uzito mkubwa.
Prof. Mkumbo amesema TBS na FCC wahakikishe wanadhibiti bidhaa bandia ambazo kuwapo kwa bidhaa hizo, kunaathiri uchumi na upatikanaji wa kodi.
Amesema licha ya ubunifu anaofanya mwekezaji huyo wa kuboresha mifumo, amesema wahakikishe vijana wanapata ajira ili kusaidia serikali.
Amesema hoja ya Mulokozi ya mabadiliko ya sheria kuwa na athari kibiashara kuanzia Februari, mwaka huu, ameelza kuanzishwa chombo cha kusimamia masuala yote ya uwekezaji na sheria itabadilika.
"Mabadiliko ya mara kwa mara ya sera na sheria tunazifanyia kazi na serikali itaendelea kumuunga mkono mwekezaji, ili afanikiwe," amesema
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, akitoa taarifa yake amesema ulipaji wa kodi umekuwa ukiongezeka kila mwaka, 2022 walilipa Sh. bilioni 7.7; mwaka 2023; Sh. bilioni 7.9 na mwaka 2024 wamelipa kodi Sh. bilioni nane.
Mulokozi amesema wako wafanyakazi 269 na wakudumu ni 147 na vibarua ni 122.
Mkurugenzi huyo amesema changamoto waliyonayo ni kukosa chupa kutoka kiwanda cha Kioo Limited na kulazimika kuagiza chupa kutoka Kenya au Oman.
Ameitaja changamoto nyingine ni uwapo wa bidhaa bandia, mabadiliko ya sera na Sheria ya Kodi, ambayo inawalazimu kulipa kodi kabla ya uzalishaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED