Heche: Mbowe ni baba yangu lakini kwa sasa akae chini

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 05:11 PM Jan 05 2025
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche.
Picha:Vitus Audax
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amechukua na kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa huku akitangaza kuwa huu ni mwisho wa utawala wa Mwenyekiti wa sasa wa Chama hicho, Freeman Mbowe.

Heche ametoa kauli hiyo leo akiwa mjini Mwanza alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati Kuu, wanachama wa CHADEMA, pamoja na waandishi wa habari kuhusu dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza kwa heshima kubwa, Heche amesema anamuheshimu sana Freeman Mbowe kama baba yake wa kisiasa na mlezi wake, akisisitiza kuwa hata katika mazingira ya ushindani hatoweza kumkosea heshima kwa namna yoyote ile.

"Mbowe amekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha demokrasia ya taifa letu na ndani ya CHADEMA tangu akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa hadi nafasi yake ya sasa. Hawezi kupingwa mchango wake wa kuwainua na kuwaibua vijana kisiasa," amesema Heche.
1

Ameongeza kuwa Mbowe anatakiwa sasa kukaa na kushuhudia kazi ya vijana aliowaandaa kwa muda mrefu, akisema:

"Yeye ndiye ametufunza na kutulea katika misingi imara. Sasa atuachie nafasi ya kutekeleza yale aliyotufunza. Muda umefika, biblia inasema kila jambo lina wakati wake, na huu ni wakati wetu."

Kwa mujibu wa Heche, upepo wa kisiasa ndani ya CHADEMA kwa sasa uko upande wa mabadiliko, ambapo wengi wanatamani kumuona Tundu Lissu akiwa Mwenyekiti wa Chama hicho ili kuleta uhai mpya wa kisiasa ndani ya chama.

2

Aidha, Heche amependekeza kuwa Freeman Mbowe asiachwe kando kabisa, bali apewe nafasi ya kuwa Mjumbe wa Kudumu wa Kamati Kuu ili aendelee kutoa busara zake kwa viongozi wapya watakaochaguliwa.

"Mimi ninamuheshimu sana Freeman Mbowe na ninampenda. Kwangu yeye ni baba wa kisiasa ambaye amenijenga hadi hapa nilipo. Siwezi kusema lolote baya juu yake. Lakini leo nasema rasmi, Mwenyekiti Freeman Mbowe, kwa heshima, tutakwenda kwenye uchaguzi, na tutakushinda kwa njia ya kidemokrasia," amesisitiza Heche.