Kinamama waliong'ara uchaguzi wa mitaa wataja yaliyowabeba

By Grace Mwakalinga , Nipashe Jumapili
Published at 01:47 PM Jan 05 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi

WANAWAKE waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka jana, wameeleza uzoefu wao kwenye harakati za kisiasa, wakitaja uthubutu kama silaha ya kwanza.

Akizungumza katika kongamano lililofanyika jijini Dar es Salaam kujadili ushiriki wa wanawake katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Myegedi kilichopo mkoani Mtwara, Rukia Myachi, alisema alikutana na vikwazo vingi ikiwamo mitazamo potofu kuhusu wanawake kuongoza.

Alieleza kuwa nyingine ni ukatili wa kijinsia, rushwa ya ngono na ukata wa fedha, lakini alijitahidi na kuvumilia hadi kufikia mafanikio.

"Nilikutana na vikwazo vingi, ikiwa ni pamoja na mitazamo potofu kuhusu ushiriki wa wanawake katika kugombea nafasi za uongozi, ukata wa fedha, na ukatili wa kijinsia kama vile rushwa ya ngono, lakini nilivumilia," alisema Rukia.

Alisisitiza kuwa uvumilivu wake ulithibitisha kwamba wanawake wana uwezo wa kuongoza kwa ufanisi, akawahamasisha wanawake wengine wasiache kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, badala yake wainuke na kuchukua nafasi za maamuzi ili kuwakilisha sauti za wenzao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Tabirugu kilichopo wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma, Leokadeki Koku, alisisitiza umuhimu wa muungano wa wanawake katika kuleta mabadiliko, akisema wanahitaji kusaidiana na kuhimiza usawa wa kijinsia katika uongozi.

Koku aliongeza kuwa ili wanawake wengi zaidi washike nafasi za uongozi, ni muhimu kuwepo na programu zinazotoa mafunzo ya uongozi kwa vijana, ili kuwawezesha kushiriki katika siasa na kufanikiwa licha ya vikwazo vya kijinsia.

"Najivunia kuwa sehemu ya mabadiliko haya na nimedhamiria kuhamasisha wenzangu kugombea, ili kuleta idadi kubwa ya wanawake katika nafasi za uongozi," alisema Koku.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mpango wa Mitandao ya Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali, alieleza furaha yake kuhusu ongezeko la wanawake katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.

Akilimali alisema kwamba, licha ya changamoto zilizokuwepo, wanawake wengi walifanikiwa kushika nafasi za uongozi katika maeneo yao.

"Nashukuru kuona mwitikio mkubwa wa wanawake kugombea nafasi za uongozi, na kwa mara ya kwanza, wanawake wamepata nafasi ya kuwa viongozi wa vijiji," alisema Gemma.

Akilimali aliongeza kuwa wanawake 14 kutoka maeneo mbalimbali walifanikiwa kushika nafasi za uenyekiti wa vijiji katika uchaguzi huu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisisitiza kuwa idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi, hasa ngazi za Serikali za Mitaa, bado ni ndogo.

"Idadi hiyo ni ndogo sana. Lazima tufanye juhudi kubwa zaidi, hasa katika ngazi za Serikali za Mitaa," alisema Lilian.

Aliwahimiza wanawake kuungana, kubomoa vikwazo vya kijinsia na kushinikiza sera zinazowawezesha kushika nafasi za maamuzi.

Lilian alikumbusha mafanikio yaliyopatikana tangu Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 na kutaja viongozi wa wanawake kama Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge Anne Makinda, na Dk. Tulia Ackson kama mifano ya mafanikio ya wanawake katika uongozi.