KARIBU tena msomaji wangu tuendelee yanayojiri kwenye anga la Maisha Ndivyo Yalivyo. Tuko mwanzoni kabisa wa mwaka mpya 2024. Ni mwaka ambao watu wengi wana mipango na malengo mbalimbali kwa maendeleo yao na taifa kwa jumla.
Mwaka ulioisha wa 2023 wengi walikuwa na pilikapilika mbalimbali za kimaisha, ikiwamo ndoa nyingi kufungwa kwa wale waliokuwa na shauku ya kupata wenza wao. Wengi walifanikisha na matarajio yakiwa ni kutengeneza familia zilizo bora.
Hebu leo niongee kidogo na wanandoa hawa. Yapo mengi watu hujifunza ambayo hawajawahi kuyasikia popote, na wanaendelea kujifunza. Baadhi ni yafuatayo;-
Ndoa ni taasisi isiyokuwa na mzoefu au mwenyeji. Ni taasisi ambayo haina kufuzu na kwamba kama ukimweka Mungu pembeni hata kwa dakika moja, kila kitu kitaharibika.
Ni taasisi inayopingwa na shetani na mawakala zake kuliko taasisi nyingine yoyote maana anajua akishavuruga ndoa, familia jamii, nchi na hata ulimwengu utaathirika.
Msomaji wangu, ndoa ni mbio ndefu na siyo mbio fupi. Ni taasisi ambayo bila neema na huruma za Mungu kuwaatamia hamuwezi kupiga hatua yoyote.
Ni taasisi inayohitaji upendo wa matendo na siyo nadharia au maneno matupu! Ni taasisi pekee ambayo hakuna kuchekana wala kunyoosheana vidole.
Inahitaji kuombeana na kutiana moyo kwa namna ya kipekee maana hakuna mwanaume au mwanamke mwenye akili timamu anayeingia kwenye ndoa akiwa na wazo la kuja kuachana baada ya muda fulani.
Ndoa ni maisha halisi na wala siyo tamthilia au maigizo. Ndoa haiwezi kudumu kama hakuna uvumilivu wa dhati na kujituma kwa pande zote mbili.
Ni taasisi ambayo lazima ujifunze kusamehe hata kama wewe hutaombwa msamaha. Ni taasisi isiyohitaji ushabiki ila maombi tu. Hili ni jambo la muhimu sana!
Ni rahisi sana mtu aliye nje ya ndoa (hajaoa/hajaolewa), kukosoa, kutukana, kukejeli ndoa ya mtu mwingine. Na pengine kujifanya bingwa wa kushauri ndoa ya wengine. Lakini mtu huyu akiingia kwenye ndoa anakuwa mpole na mkimya kabisa.
Kila mtu anaingia kwenye ndoa kwa staili yake. Kila mtu anaoa au anaolewa na mtu wa aina yake tofauti na mwingine.
Kila mtu anaoa au olewa na mtu mwenye tabia tofauti, akili tofauti, msimamo tofauti, harufu tofauti na asili tofauti. Hivyo, bila uvumilivu na upendo wa kweli, unaweza kuchoka haraka sana.
Kwenye ndoa kuna majira ya kucheka na kufurahi. Kuna wakati ndoa inakuwa tamu kama asali, lakini kuna nyakati ndoa inakuwa chungu zaidi ya mwarobaini kiasi cha kutamani kurudi kwenu.
Lakini katika hali zote hizo kitakachoweza kuwasimamisha ni uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana na kuachilia, kusitiriana na zaidi maombi ya neema.
Ndoa si kitu cha kujingamba, kujitapa na kujitutumua kuwa una ndoa nzuri kuliko wengine. Ndoa siyo kitu cha kujifanyia mashindano na jirani yako. Siyo sehemu ya majaribio, ni taasisi ya kuheshimiwa na kuombewa.
Mungu akikupa ndoa nzuri, mshukuru na ombea wengine ambao ndoa zao zinapitia tafrani mbalimbali. Wengi kutokana na kukosa uvumilivu, ndoa zao zimesambaratika. Zipo zilizoishia kuvunjika mahakamani, wengine wametengana kila mtu anaishi kivyake.
Lakini, kama nilivyotangulia kusema hakuna mtu anayeingia kwenye ndoa kwa matarajio ya kuachana muda mfupi ujao. Wanakuwa na malengo na maono katika kufanikisha safari yao ya ndoa.
Msomaji wangu, kuingia katika ndoa kunahitaji umakini mkubwa sana. Mshirikishe kwanza Mungu atangulie safari yenu. Wengi walikurupuka wakaishia njiani ndoa zikiwa changa kabisa. Wakasahau kwamba wanapoandaa mipango yao ya maisha, adui naye yupo kazini akipanga mbinu za kuwaharibia.
Hata ndoa zilizodumu muda mrefu na kwa mafanikio makubwa, shetani haachi kuzivuruga. Hayo ni majaribu lakini kwa wanaomtumaini Mungu, huwasaidia kushinda yote.
Ndio maana katika moja ya maandiko yake anasema hakuna jaribu lisilo na mlango wa kutokea. Utatikiswa lakini usikate tamaa kwani njia ya kutokea ipo ukiwa mvumilivu.
Wengi wanakosa uvumilivu wanazikimbia ndoa zao hata kwa mambo madogo madogo. Lakini mambo yakizidi huku ukimtumaini Mungu, Yeye hufanya mlango wa kutokea, na kukuokoa.
Wiki ijayo nitawapa mfano wa ndoa hizi. Je, una maoni, Kisa? Ujumbe 0715268581.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED