Makalla: afunda wanafunzi kutimiza ndoto ya Rais nchi kuwa na wasomi

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 08:43 PM Jul 14 2024
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa,  Amos Makalla akiongea na wanafunzi.
Picha: Romana Mallya
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla akiongea na wanafunzi.

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amewaeleza wanafunzi wa shule ya mchepuo wa sayansi ya Dar es Salaam Girls High School iliyoko Wilaya ya Ubungo ambayo ni miongoni ambazo zinajengwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wanatimiza ndoto ya Mkuu wa Nchi kwa kutopata mimba au kuwa watoro.

Amesema  hayo leo Mkoa Dar es Salaam katika mwendelezo wa ziara yake mkoani humo ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa.

Amesema shule hiyo haitokuwa na maana kama wanafunzi hawatotimiza kusoma ili kutimiza ndoto alizoziweka Rais Samia katika shule hizo.

"Ninajua hapa wapo mawaziri, wakuu wa mikoa, mabalozi wa nchi mbalimbali, madaktari na walimu, tunataka watoke katika shule hii, ninaamini hatutosikia utoro wala mimba," amesema.

Wanafunzi.

MRADI WA MAJI

Katika ziara hiyo, Makalla amekagua mradi wa tanki la maji lita 6000 la Mshikamano, lililopo Mshikamano, wilaya ya Ubungo na kuagiza kasi ya usambazaji wa huduma hiyo iongezwe.

"Ni dhahiri kwa miradi hii ya kisasa na yenye tija kwa jamii tukianzia mradi huu wa maji hapa Jimbo la Kibamba wa tanki la maji la ujazo wa lita 6000 ambao unaenda kusambaza maji safi na salama Jimbo la Kibamba na Wilaya ya Ubungo ni kielelezo tosha kuwa Ilani inatekelezwa, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amesimamia vizuri utekelezaji," amesema.