Waziri Mkuu amfagilia Samia utekelezaji miradi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:55 AM Mar 31 2024
Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
PICHA: CCM
Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ni kinara na kielelezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoigusa jamii ya watanzania.

Majaliwa amesema maono na misingi iliyojengwa na Rais Samia imewezesha serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya kimkakati na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.

Akizungumza katika kongamano la Maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Samia lililofanyika mkoani Mwanza, Majaliwa amesema serikali imetekeleza miradi ya usafiri katika Maziwa Makuu.

“Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha usafiri wa anga, usafirishaji kwa njia ya reli, barabara na usafiri katika bahari na maziwa makuu,” amesema.

Amesema miongoni mwa miradi ni mradi wa ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori matatu na hadi sasa umefikia asilimia 94 ya ujenzi wake.

 Amesema serikali pia imefanya maboresho katika bandari na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika bandari hizo ikiwamo bandari kwenye Ziwa Victoria. 

Pia amesema katika kuimarisha sekta ya kilimo, serikali imeendelea kuboresha usimamizi na utoaji wa huduma kwa kuongeza bajeti katika Wizara ya Kilimo.

“Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa zao la pamba ikiwamo kuongeza thamani ya zao hili. Nitoe wito kwa wakulima wa zao hili, kuongeza uzalishaji ili mahitaji tuliyo nayo yaendane na uhitaji uliopo,” ameagiza.

Kadhalika, amesema serikali inaendelea na ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi pamoja na kutoa zana bora, pembejeo na vifaa muhimu vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi, lengo ni sekta hiyo kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Zimenunuliwa na kusambaza boti 160 za kisasa za uvuvi zenye thamani ya Sh. bilioni 11.5 kwa vyama vya ushirika wa wavuvi, watu binafsi na vikundi vya wavuvi katika halmashauri 58,” amesema.

Katika hatua nyingine, Majaliwa ametoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa za uwekezaji zilizowekwa na serikali ili kukuza uchumi wa taifa na mtu binafsi.