Wanawake wataka masuala ya kijinsia, uwajibikaji Dira 2050

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 02:44 PM Jul 14 2024
Mwenyekiti wa TGNP, Gemma Akilimani.
Picha: Maktaba
Mwenyekiti wa TGNP, Gemma Akilimani.

WAKATI nchi ikiwa katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, wanawake wamesema masuala ya kijinsia yawekwe yanapaswa kuzingatia kila sehemu.

Wamesema kuwekwe utaratibu shule zote zitoe taulo za kike bila malipo na kujengwe misingi ya uwajibikaji dhidi ya ubadhirifu wa rasilimali za taifa.

Hayo yalibainishwa juzi katika kongamano la kitaifa la wanawake kuhusu ukusanyaji maoni ya Dira ya 2050 lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), wajumbe wa Tume ya Mipango na Uratibu (TDV2050) ilikuwa miongoni mwa walioshiriki.

Kongamano hilo, pamoja na mambo mengine, limelenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu suala hilo na mchango wake kwa maendeleo ya wanawake.

Akifungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa TGNP, Gemma Akilimani, alitaja mambo ambayo wanatakiwa kuyatilia maanani ni pamoja na kuja na mabadiliko ya yale yaliyotiliwa mkazo kupitia mpango huo.

Alisema wanatazamia sekta zote zijikite katika mchakato utakaobainisha masuala ya kijinsia katika mpango huo, bajeti na utekelezaji wake.

"Kwa maandishi tunaweza kukuta suala la jinsia limetajwa kama kipengele tu, ukweli ni lazima masuala ya kijinsia yawekwe katika kila mchakato.

"Hii inamaanisha kwamba, kufanya uchambuzi wa kina wa masuala hayo ikiongozwa na takwimu zinazokidhi mipango na ugawaji rasilimali.

"Hakuna kinachowezekana kutekelezwa bila kuzingatia masuala ya kijinsia katika mipango ya bajeti," alisema.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Anna Kulaya, alisema ili kuwa na mrengo huo lazima madai yao yazingatie.

"Sisi ndio tunaoandika dira na tunaamini tunayozungumza hapa yatabebwa kwa uzito wake. Ushiriki wa wanawake hata huko nyuma ni mdogo sana, tunaamini tunapozungumzia suala la wanawake  tulibebe kwa uzito wake na madai tunayotaka yaweze kuingia katika dira," alisema.

Anna alitaja maoni ya wanawake watakayo ili kuingizwa katika Dira 2050, ni mchakato huo uendelee kuwa shirikishi na jumuishi, ili iwe yenye mrengo wa kijinsia.

Kuhusu maisha bora na mazuri, Anna alisema ifikapo mwaka 2050, wanadai kusiwapo kaya itakayokuwa na ukosefu wa chakula bora na cha kutosha au watoto na watu wazima wenye matatizo yatokanayo na lishe.

Anna alisema elimu inayotolewa iwe  ya kumkomboa mwanamke kudai haki zake na kumwezesha kujisimamia na kutumia vipaji vyake kama raia huru.

"Jamii na mitazamo inayohalalisha ubaguzi wa kijinsia, tunataka dira inayokuja iweke elimu itakayosaidia wanawake na jamii kuzingatia masuala haya.

"Kuhakikisha shule zote zinatoa taulo za kike bure kwa sababu inasikitisha unapoona bajeti katika vitu vyenye kodi, taulo za kike zinaletewa kodi. Ni adhabu wanawake kuingia hedhi kwa mwezi?

"Kwanini ziwekewe kodi au masharti magumu? Tunahitaji taulo za kike zitolewe bure kama moja ya zana ya elimu kwa sababu ni haki," alisema.

Alisema suala la usawa wa kijinsia liingizwe katika maeneo yote ya Dira 2050 ikiwamo kwenye utangulizi, malengo, utekelezaji, ufuatiliaji wake waone sekta zote zikiwamo uchumi, uongozi, siasa, umiliki wa rasilimali na ufanyaji uamuzi kote kuwekwe.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, katika uchambuzi yakinifu wa Dira 2020/25, alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, aliwahi kukiri kwamba dira haitakuwa na maana yoyote wala maendeleo endapo kila mtu hatawajibika kuimarisha umoja na utengamano.

"Kwetu wanamtandao tamko hili la Rais Mkapa ni msingi elekezi ambao tunatarajia uendelee kuingizwa na kusimamia masuala ya usawa wa kijinsia sehemu zote muhimu za dira, kinyume chake utaathiri utekelezaji wake," alisema.

Dk. Amina Msengwa kutoka Tume ya Mipango na Uratibu (TDV 2050), aliwaeleza wanawake kwamba wataendelea kushirikiana kwa karibu, huku akiwaeleza namna ya kujaza dodoso.

Dk. Florence Turuka kutoka tume hiyo alisema  wakijilinganisha walikotoka, mabadiliko mengi yametokea, akitolea mfano mwaka 2000 walikuwa hawazungumzii mabadiliko ya tabianchi, ndio maana lazima wafikirie mabadiliko yaliyojitokeza katikati nini kifanyike.