Wakulima wahakikishiwa mbolea msimu huu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:22 PM Feb 08 2026

Wakulima wa Mbozi kwenye mkutano huo
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakulima wa Mbozi kwenye mkutano huo

Serikali inatarajia kuwapatia wakulima wilayani hapa Mkoa wa Songwe mbolea kupandia, kukuzia na kubebeshea kwa msimu huu wa kilimo kwa wingi na kwa wakati.

Hatua hiyo inakuja baada ya kubaini zaidi ya tani 3,544 za mbolea zinauzwa katika maduka ya wafanyabiashara waliothibitishwa. 

Ni baada ya kutuma wataalam wake kilimo kufanya uchunguzi kwenye mashamba ya baadhi ya wakulima hao  wilayani hapa kuhusu mbolea aina ya DAP kupitia mfumo rasmi wa ruzuku.

Kabla ya uchunguzi huo, wataalamu hao wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, wametoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo.

Vilevile, wametoa elimu ya umuhimu kwa wakulima kununua mbolea kupitia mfumo wa ruzuku kwa kutumia namba za mkulima, kuchagua mbolea sahihi kulingana na hatua ya ukuaji wa zao, hususan kwa mazao yaliyoingia hatua ya kuweka mbolea ya kukuzia.

Mafunzo hayo yalitolewa kwa wakulima 541 wa kata za Mahenje, Halungu, Magamba na Itaka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.

Mafunzo hayo ni umuhimu wa kupima afya ya udongo kabla ya matumizi ya mbolea ili kumwezesha mkulima kutambua virutubisho vilivyopo na vinavyokosekana kwenye udongo, kuchagua mbolea inayofaa na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Ofisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka hiyo, Chrysanthus Funda, amesema kupima sampuli ya udongo humsaidia mkulima kuchagua mbolea sahihi na kuepuka matumizi ya mbolea isiyofaa  kwa kutofanya kazi ipasavyo. 

Ofisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka hiyo, Mushoborozi Christian, amewahimiza wakulima kuhakikisha wanasajili na kuhuisha taarifa zao katika mfumo wa ruzuku ya mbolea.

Christian, amesema  usajili huo ni msingi wa mkulima kupata pembejeo kwa wakati, kwa bei nafuu na zenye ubora unaothibitishwa na serikali. 

Amesemaa kununua mbolea nje ya mfumo rasmi, huwaweka wakulima katika hatari ya kupata isiyokidhi viwango na kusababisha hasara na kushuka kwa uzalishaji.

Amesema wanaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji wa mbolea nje ya mfumo rasmi, ikiwemo kufutiwa leseni.

Yohana Kibona, Mkulima wa Halungu, amewashukuru wataalamu hao kwa kuwapa mafunzo hayo na kuwaongezea uelewa kuhusu mbolea bora na umuhimu wa kununua pembejeo kupitia mfumo rasmi wa ruzuku.