Vijana waagizwa kulinda taswira ya nchi kimataifa

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:35 PM Feb 08 2026
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo akizungumza na vijana  Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga rasmi vijana 200 wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo akizungumza na vijana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga rasmi vijana 200 wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi

Serikali imewataka vijana wanaopata fursa za ajira nje ya nchi na kuwa mabalozi wa taifa, kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na tamaduni katika nchi wanazokwenda, ili kulinda heshima ya Tanzania.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo, amesema hayo Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga rasmi vijana 200 wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kisuo amesema serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ya kusimamia ajira nje ya nchi, kwa lengo la kuhakikisha watanzania wanapata ajira zenye staha.

Ameeleza kuwa, serikali imeendelea kuratibu na kusimamia shughuli za Mawakala Binafsi wa Ajira waliosajiliwa, ambao wanawaunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira, Jane Sorogo, amewashukuru Mawakala Binafsi wa Ajira, kwa namna wanavyoshirikiana na serikali katika kuwaandaa vijana wanaopata fursa za ajira nje ya nchi.

Makamu Mwenyekiti wa Mawakala wa Ajira nchini, Rashid Milao, ametoa wito kwa vijana waliopata fursa hizo za ajira kuzingatia maelekezo waliyopewa na serikali, ili kuiwakilisha vyema Tanzania kimataifa.