Shule mpya ya sekondari ya amali ya mkoa wa Njombe, iliyopo wilayani Ludewa, imeanza rasmi kupokea wanafunzi ambao wameanza masomo, hatua inayotekeleza azma ya serikali, kuhakikisha kila mkoa unakuwa na shule ya amali.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ludewa shuleni hapo, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, amesema ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuimarisha elimu ya mafunzo kwa vitendo nchini.
Ameeleza kwamba hata kabla ya wanafunzi kuanza masomo, serikali ilikuwa tayari imeshapeleka walimu wa fani mbalimbali, akimpongeza Rais kwa hatua hiyo ya mapema ambayo imewezesha kuanza kwa masomo bila kuchelewa.
Mkuu huyo wa wilaya amesema, shule hiyo imejengwa karibu na eneo lililopangwa kuwa kongani ya viwanda, ikiwemo kiwanda cha saruji, kiwanda cha kuchakata chuma, pamoja na kiwanda cha kutengeneza vifaa na vipuri vya chuma kama koili, nondo. 
Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Mikael Hadu, akisoma taarifa ya ujenzi amesema shule ya sekondari Ulayasi, imepokea shilingi bilioni 1.6 na lengo la mradi ni kusogeza huduma ya elimu ya mafunzo kwa vitendo kwa wananchi na kufanikisha azma ya kila mkoa kuwa na shule ya sekondari ya amali.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ludewa, Stanley Kolimba, amepongeza ujenzi wa shule hiyo, akisema utachochea ujuzi kwa vijana na kupunguza changamoto ya ajira katika eneo hilo.
Ujenzi wa ya amali mkoani humo, unatajwa kuwa hatua muhimu ya kuunganisha elimu na mahitaji halisi ya soko la ajira, hasa katika sekta ya viwanda inayotarajiwa kukua wilayani Ludewa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED