THDRC yatoa neno mauaji albino, utekaji watoto

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 10:31 AM Jul 28 2024
THDRC yatoa neno mauaji albino, utekaji watoto.
Picha: Mpigapichga Wetu
THDRC yatoa neno mauaji albino, utekaji watoto.

KUTOKANA na kukithiri kwa matukio ya kupotea na mauaji ya watu wenye ualbino nchini na utekeji wa Watoto, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), wameitaka serikali kuwajibika katika kuhakikisha wanaweka mazingira imara ya kudhibiti matukio hayo.

Kauli hiyo ilitolewa juzi katika tamko lililohusisha wajumbe 55 kutoka Kanda ya Ziwa, Magharibi na Mashariki, wakiitaka serikali kupitia vyombo vyake kusimama katika misingi ya kiutendaji ili kuweka nchi salama.

Mratibu wa Mtandao huo Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Donald, alisema pamoja na mambo mengine, tamko hilo linakwenda sambamba na kuitaka serikali kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine kudhibiti matukio yote ya utekaji wa watoto, watu wazima, kupotea kwa watu na mauaji ya watu wenye ualbino.

“Kwa kauli ya pamoja tunakemea vitendo hivi na kuiomba serikali kuweka mkazo katika kukabiliana navyo kwani umekuwa mwendelezo kila ifikapo kipindi cha uchaguzi,” alisema.

Kuhusu matukio ya utekaji na mauaji kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla, mjumbe wa mtandao huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko, alisema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi kwa mwaka 2003, watoto 73 walitekwa nchini.

Alisema kati ya watoto hao, 33 walitekwa kutoka Kanda ya Ziwa na kuwa kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2024, walitekwa watu 20 wenye ualbino katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huku mwaka huu yakitokea matukio matatu kwa mkupuo.

“Tulishuhudia Mei 4, mwaka huu, tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa mtoto Kazungu Julius huko Geita. Mei 30, alitekwa na kuuawa mtoto Asimwe huko mkoani Kagera na kifo cha Mathias Sangoma aliyekatwa mkono na kuvuja damu nyingi huko Kwimba mkoani  Mwanza.

“Mwingine ni mtoto Happyness Raphael, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustiono (SAUT) Mwanza aliyevamiwa na kushambuliwa kwa mapanga na watu wasiyojulikana. Tukio  lingine ni la Juni 25, mwaka huu, huko wilayani Sengerema ambako kijana Liyani Donald alivamiwa akiwa amaelala na kufanikiwa kujinasua,” alisema Soko.

Mjumbe Mwingine Musa Jonas alisema matukio hayo yamekuwa yakitokea zaidi katika vipindi vya uchaguzi hali ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara huku akiitaka hali hiyo iikumbushe serikali juu ya kuweka nguvu ya pamoja katika kukabiliana nayo.

Alisema kuendelea kwa matukio hayo ni ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 14, Mkataba wa Kimataifa wa kuhusu watu wenye ulemavu wa mwaka 2006,  Tamko la Dunia  juu ya haki za binadamu la mwaka  1948 na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu la mwaka 1981.

Kuhusu matakwa ya mtandao huo, Mjumbe wa THRDC, Sophia Nshush,i alisema wanalitata Jeshi la Polisi kuwajibika kwa kuchukua hatua juu ya matukio hayo ili kuyakomesha moja kwa moja pamoja na kutoa taarifa kwa umma mapema pindi yanapotokea katika jamii.

Pia alisema mtandao huo unamkumbusha Rais Samia Suluhu Hassan kuunda kamati huru ya kushughulikia masuala hayo kwa kuwa tangu yameanza, hakuna chombo kilichoundwa kwa ajili ya kudhibiti na kuyatolea taarifa rasmi.

“Tunaiomba serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kumaliza haraka mchakato wa upitishwaji wa rasimu ya Mpango Kazi wa  Taifa wa Watu Wenye Ualibino wa mwaka 2023/24 mpaka 2027/28 ili hatua za utekelezaji zianze kuchukuliwa,” alisema Nshushi.

Pia alisema serikali inatakiwa kutenga bajeti maalum ili kuimarisha mifumo ya ulinzi kwa watoto na watu wenye ualibino kuanzia ngazi za vitongoji hadi taifa ili kuwa na ulinzi madhubuti.