MAMBO magumu na mazito wanayopitia watoto wanaojilea wenyewe mitaani si ya kupuuzwa. Wako wanaobakwa, kuingizwa katika magenge ya uhalifu na wengine huishia kuwa waraibu wa dawa za kulevya.
Wanalala katika mabaraza ya maduka, mapagala, magari mabovu na wengine hutumikishwa kingono usiku kucha.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Manyara, Kilimanjaro, Shinyanga na Dodoma, umebaini watoto hao wanawafahamu wazazi wao na ndugu na wana visa vinavyofanana vilivyochangia kuwa mtaani.
Visa tajwa ni pamoja na ugumu wa maisha nyumbani, vipigo na ugomvi wa mara kwa mara wa wazazi unachangia kuwapo mazingira hatarishi.
Wakati jamii ikiwatazama kwa mtazamo hasi na pengine kuwahukumu kwa matendo yao mtaani, watoto hao wanalindwa na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto 1990 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu 1989.
SAUTI ZAO
Baadhi ya simulizi zao ni pamoja na ya mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 11 (jina linahifadhiwa) anayesimulia kwamba: “Kulala kwenye mabaraza ya watu ni maisha yetu ya kila siku, hatupendi maisha haya, kikundi chetu tupo kama watano, wakike wako wawili. Tunalala pamoja huwa tunatandika maboksi chini tunayalalia.
“Asubuhi mpaka jioni huwa tunazunguka katika mitaa yenye watu wengi au kwenye foleni za magari, tunaomba fedha.Niliondoka nyumbani baada ya mateso ya ndugu wa baba, sina wazazi wamefariki dunia.
“Katika kuomba wapo wanaotupa Sh. 100, Sh. 200 na wengine buku (Sh. 1,000), nikikosa mimi atapata mwenzangu, tunanunua chakula tunakula haya ndio maisha yetu huku Kariakoo.”
Mtoto huyo mwenyeji wa Kagera, anasema changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na wakati mwingine kutaka kugongwa na magari, pikipiki au bajaji na nyakati za usiku baadhi yao kuna watu wazima wanawadhalilisha kingono na wengine wanavuta sigara na gundi.
Maisha ya mtoto huyo hayatofautiani na ya binti mwenye miaka 12 (jina linahifadhiwa) aliyekutwa Kituo Kikuu cha Mabasi Moshi, anayesimulia kuwa alikimbilia mkoani humo akitokea Morogoro.
Anasema alikimbia baada ya mjomba wake (jina tunalo), kumtishia kumuua baada ya mama yake mzazi, (jina tunalo) kuolewa mkoani Katavi.
"Tulikuwa tunaishi vizuri na mama na mjomba na bibi, baba yangu simjui ila mama alipata baba mwingine na wakaondoka kwenda Katavi.
“Mjomba akaanza kunitesa kwa kumwambia bibi maneno ya uongo, siku moja alinitishia kuniua na panga, nikatoroka na kulala kwenye shimo la mchanga na asubuhi nikaanza safari hadi nikajikuta huku.
“Tunalala popote katika maeneo ya stendi kwenye mwanga ili wale wakaka wakorofi wasije wakatufanyia vitendo viovu. Tupo wadada watatu ila huyo mwingine amehamia Njiapanda,” anasimulia.
Mtoto mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) anayetokea jijini Tanga anasema: “Wako wenzetu wanaotumika kwenda kufanya matukio ya kuvunja na kuiba na wengine wanachukuliwa na wasamaria wanapelekwa kwenye vituo na wengine tunaachwa.”
Mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 15, aliyetoroka nyumbani kwao akiwa na miaka 10 na ku
kimbilia Arusha na baadaye Dar es Salaam, anasema akilinganisha maisha ya mtaani na nyumbani alikotoka, anaona bora aliko sasa kwa sababu amekuwa akipigwa sana na mama wa kambo.
Mtoto mwingine wa kiume mwenye miaka 12 aliyekutwa Ubungo akiomba anasema: “Novemba, 2023 nilitoroka nyumbani baada ya wazazi kunilazimisha kwenda shule. Nisipokwenda wanafunzi walikuwa wanatumwa nyumbani na kunipeleka shule na huko nilichapwa sana, nikaamua kutoroka na wenzangu kuja huku.”
Anasema kazi anazofanya sasa ni vibarua kama kufagia, kuuza vitafunwa na kuosha vyombo kwenye migahawa midogo ili kupewa fedha za kujikimu.
Mtoto mwingine wa kiume mwenye miaka 11 mwenyeji wa Ukerewe, anasema aliondoka nyumbani mwaka 2017 akiwa na miaka sita kutokana na ulevi uliokidhiri wa mjomba aliyekuwa akiishi naye baada ya wazazi wake kufariki dunia.
Binti wa miaka 16 aliyekutwa eneo la Mji Mpya, Dodoma akiomba fedha kwa wapita njia, anasema alikimbilia mtaani akitokea wilayani Bahi, kutokana na ugumu wa maisha baada ya mama yake kumtelekeza kwa bibi yake.
Anasimulia ugumu wanaoupata usiku ni kulala kwenye mabaraza ya maduka huku baadhi ya watoto wenzao wenye umri mkubwa kuwaingilia kimwili.
WENYE MADUKA
Mfanyabiashara wa duka la vinywaji Ubungo, Dar es Salaa, Isakwisa Mwakasege, anasema watoto hao wamekuwa wakilala nje ya maduka katika eneo hilo likiwamo la kwakwe.
Mwakasege anasema watoto hao wenye umri kati ya miaka 10 hadi 15, ambao ni wengi, mbali ya hilo wamekuwa wakijihusisha na matumizi ya pombe kali, sigara na uvutaji gundi.
“Tukiwahoji wanapajua nyumbani kwao, ukiwaambia warudi nyumbani wanasema, ‘bora tufie barabarani’, inaonekana nyumbani kwao kuna shida,” anasema.
Maria Paul, mkazi wa Mbauda, jijini Arusha, ambaye ni muuzaji wa mboga, anasema kila alfajiri wakati akienda sokoni kupeleka bidhaa zake, njiani hukutana na watoto wamelala vibarazani.
Naye, Juma Hassan, mkazi jijini humo, anasema kutokana na watoto hao kuishi muda mrefu mtaani kwa kujilea wenyewe, baadhi yao wamekuwa na tabia ambazo mtu akiwaingia bila tahadhari wanaweza kumdhuru.
Monica Boniface, mkazi wa Kawe, Dar es Salaam, anasema watoto hao wana ndoto kubwa za maisha yao baadaye, lakini wanakosa msaada wa kuelekezwa kwenye njia iliyo sahihi na salama.
VIONGOZI WA DINI
Padre wa Kanisa Anglikana Kigogo, Joseph Upio, anashauri wazazi kutenga muda wa kukaa na watoto wao na kuwaonesha upendo, kwani kinyume na hapo hali itazidi kuwa mbaya.
Pia anahimiza wanandoa kuzingatia viapo vya ndoa, kuishi na maadili, mavazi yenye staha, na kutunza usiri wa mambo ya familia ili kuwalea watoto katika misingi bora.
Ametoa wito kwa jamii kukemea vitendo viovu na kanisa kutoa mafundisho kwa wazazi na walezi ili waishi kwa misingi inayompendeza Mungu na kuimarisha familia bora.
Mchungaji wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God (EAGT), Richard Shija, anasema mmomonyoko wa maadili wa wazazi kushindwa kusimamia majukumu yao ya kulea familia unachangia ongezeko la watoto hao mtaani.
Anasema baadhi ya watoto kutokana na kukosa malezi bora, hujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu kama uporaji, ujambazi, panya road jambo ambalo ni kero kwa jamii.
Hivyo, anaishauri serikali kupitia Jeshi la Polisi kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii kuwakutanisha na wazazi na wasio nao, wapelekwe vituo vya kulelea watoto ambavyo ni salama kwao.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Elim Pentekoste Tanzania (KEPT), Peter Konki, anawashauri wazazi kubeba jukumu la malezi ya watoto wao ili kuondokana na mtoto anayeitwa wa mtaani.
Yusufu Mtobela, Mkurugezi wa Shirika lisilo la kiserikali la Uzao Wetu lililoanzishwa mwaka 2023 kwa lengo la kuelimisha jamii na wazazi juu ya malezi salama kwa watoto na kutambua vipaji vyao anasema: “Awali nilikuwa nafanya kazi katika kituo cha kulea watoto kutoka mitaani na kuwarudisha nyumbani kwao pindi wanaporidhia na hutoa elimu kwa jamii.
“Nilichobaini ni kwamba, ushirikishwaji wa jamii pamoja na elimu kwa wanafamilia ndicho kitu ambacho jamii inakosa, ninashauri ni muhimu serikali kuwekeza zaidi huko ili kuzuia watoto wasiipende mitaa zaidi ya familia zao.”
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lidya Kwesigabo, anasema tatizo hilo lisipodhibitiwa mapema linaweza kutokea tatizo la wimbi la vibaka.
Anasema takwimu za watoto wa mitaani mkoani humo kwa sasa wapo 612 na wanaoishi katika mazingira hatarishi ni 99,939 sababu zikiwa ni migogoro ya ndoa, umaskini, malezi duni na uvutaji wa madawa ya kulevya.
Ofisa Ustawi wa Jamii mkoani Manyara, Hadija Muwango, anasema kuwapo kwa kundi la watoto hao mitaani ni tishio jipya.
Anabainisha kwamba changamoto wanayokabiliana nayo ni wengi wao kuwa waongo na wengine kuwa wezi na inapotokea wamewarejesha kwenye familia zao, baadhi huamia mikoa mingine.
WASAIKOLOJIA TIBA
Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Said Kuganda, amesema watoto hufuata mkombo kwa kutazama wenzao na mwisho wa siku kuhamia mitaani.
Miongoni mwa changamoto za kisaikolojia Dk. Kuganda anazitaja ni pamoja na kuathirika kiakili na kuharakisha kuelewa mambo ambayo yamepita umri wao, kutokana na mazingira magumu wanayokutana nayo mitaani.
Kadhalia anasema wanapata wasiwasi, ukatili wa kijinsia na ulevi ambazo huathiri watoto wa mitaani kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko wale wanaolelewa nyumbani.
Dk. Kuganda anatoa wito kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kutafuta njia za kuwasaidia watoto hao kwa kuwapa huduma za kisaikolojia, afya ya akili, elimu na kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu kama chakula na usalama.
Hivi karibuni, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camilus Wambura, akifunga mafunzo ya Jeshi la polisi katika Shule ya Polisi Moshi,Kilimanjaro, alisema kwa sasa kuna ongezeko la mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi na kusababisha ongezeko la watoto wa mitaani.
“Maadili yameendelea kuporomoka, wivu wa mapenzi umezidi, mauaji yanaongezeka na watoto wa mtaani wanaongezeka, hii sio dalili njema kwa taifa letu, viongozi wa dini mtusaidie na jamii tukubali mabadiliko ya kifikra,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED