Wahukumiwa jela maisha kwa kosa la kubaka watoto

By Grace Mwakalinga , Nipashe Jumapili
Published at 12:29 PM Nov 10 2024
Jela.
Picha:Mtandao
Jela.

WATU wawili wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na mwingine miaka 20 kwa makosa ya kuwabaka watoto wenye umri chini ya miaka 10 mkoani Mbeya.

Vitus Thadeo (26), mkazi wa Kata ya Mwasanga, mkoani humo amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka minane ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwasanga mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Benjamin Kuzaga, alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushahidi mahakamani ili kesi za namna hiyo kupata mafanikio.

Alisema hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Andrew Scout na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Augustino Magesa.

Alisema imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 130 na 131 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu ambapo, mshitakiwa alitenda kosa hilo mwezi Juni, mwaka huu, baada ya kumvizia na kumbaka binti huyo akiwa chumbani kwake.

Kamanda Kuzaga alisema Christopher Kidumba (55), mkazi wa Kijiji cha Kanioga wilayani Mbarali, alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka (8), mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Kanioga.

Alisema hukumu hiyo ilitolewa hivi karibuni na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbarali, Aliko Mwandumbya chini ya Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Mkaguzi Msaidizi Given Kombe.

Kuzaga alisema hukumu hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 131 kifungu kidogo cha kwanza vyote vya sheria ya kanuni ya adhabu ambapo mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari Mosi, mwaka huu, baada ya kumkamata kwa nguvu binti na kisha kumbaka na kumsababishia maumivu makali mwilini.

Mwingine ni Michael Mwaisaka (42), mkazi wa Kijiji cha Mwaya wilayani Kyela, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kumlipa fidia mwathirika kiasi cha Sh. 300,000 kwa kosa la shambulio la aibu alilolifanya kwa mtoto mwenye umri wa miaka minne, mwanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Mwaya.

Alisema hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kyela, Paul Barnabas na Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Mkaguzi Msaidizi Bihemo Mayangela.

Alisema hukumu hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 138 (C) kifungu kidogo cha kwanza (a) na kifungu kidogo cha pili (b) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 19, mwaka huu, baada ya kutengeneza mazoea na mtoto huyo na kutumia nafasi hiyo kumchukua kutoka kwa bibi yake aliyekuwa anauza ndizi karibu na klabu ya bia.

Kamanda Kuzaga alisema bibi yake hakujua na ndipo alipokwenda naye katika kichaka na kumfanyia kitendo hicho kiovu.

Kutokana na hukumu hizo, Kamanda kuzaga alivipongeza vyombo vyote vya haki jinai kwa ushirikiano unaotolewa ili kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya washitakiwa na watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya jinai.