Rais Samia amlilia Lawrence Mafuru

By Jenifer Gilla , Nipashe Jumapili
Published at 10:08 AM Nov 10 2024
Marehemu Lawrence Mafuru.
Picha:Mtandao
Marehemu Lawrence Mafuru.

KATIBU Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru, amefariki dunia akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa maradhi yaliyokuwa yanamkabili.

Kutokana na kifo hicho, Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa watumishi wa tume hiyo, ndugu, jamaa na marafiki.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Sharifa Nyanga, ilisema Rais Samia  atamkumbuka kwa utumishi wake uliotukuka, bidii na ubunifu alipotumikia nafasi mbalimbali serikalini.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Lawrence Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kilichotokea leo (jana) katika Hospitali ya Apollo nchini India,” alisema Rais Samia.

Kabla umauti, Mafuru ametumikia nchi kupitia taasisi mbalimbali. Alianza safari yake mwaka 1998 katika Benki ya Standard Chartered, akijikita katika Ufadhili wa Biashara za Kimataifa.

Kwa kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyofuata, alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi zikiwamo kuwa Msajili wa Hazina, Mtendaji Mkuu Benki ya NBC, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Nchini (TBA) na mwanzilishi Mwenza wa Kampuni ya Ushauri wa Masuala ya Fedha ya Bankable

Ubobezi wake katika masuala ya fedha ulisababisha kuombwa mara kwa mara kutoa mihadhara katika sekta hiyo.
Ofisi ya Msajili ya Hazina kwa upande wake, ilisema itamkumbuka Mafuru kwa bidii, ubunifu na unyenyekevu wake wakati wote walipofanya naye kazi katika ofisi hiyo kuanzia Novemba 5, 2014 hadi Decemba 7, 2016.

“Nasi tunaungana na Rais Samia kutoa pole kwa familia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo watumishi wa Tume ya Mipango, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia msiba huo” ilisema ofisi hiyo.