Utoaji huduma za kijamii kuboreshwa kukuza uchumi

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 12:56 PM Nov 10 2024

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale.
Picha:Mtandao
NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale.

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale amesema wanaendelea kuboresha utoaji wa huduma za jamii kwa kushirikiana na wizara za kisekta ili kukuza uchumi, kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa mwananchi mmoja mmoja na wa taifa kwa ujumla.

Mtwale aliyasema hayo jana wakati akifungua kikao kazi cha ofisi hiyo na wizara za kisekta kilicholenga kujadili uratibu wa mipango na bajeti kwa shughuli zinazotekelezwa na kusimamiwa katika ngazi za halmashauri, mikoa na wizara za kisekta.

“Kikao hiki ni fursa ya kujadili mipango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, hivyo niwaombe mshiriki kikamilifu kwa kutoa maoni na ushauri utakaowezesha uandaaji mzuri wa mipango na bajeji kwa mwaka wa fedha ujao,” Mtwale.

Alisema kikao hicho kitasaidia kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili serikali katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika ngazi za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Aliwataka washiriki kuongeza ubunifu wakati wa uandaaji wa mipango na bajeti ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi na sekta binafsi, na hatimaye kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa ambazo zitakuwa na bei nzuri katika masoko ya nje.

“Nitumie fursa hii kuendelea kuwakumbusha na kuwasisitiza mhakikishe kuwa, mnaandaa mipango na kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa afua na shughuli mbalimbali katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI,John Cheyo alisema lengo la kuandaa kikao cha wizara za kisekta ni  kujenga uhusiano mzuri kiutendaji pamoja na kuangalia namna bora ya kusaidiana katika kutekeleza shughuli za kisekta kwa wananchi katika ngazi ya chini ambayo ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

“Wizara za Nishati, Kilimo, Maji na Mifugo na Uvuvi ambazo zimewakilishwa hapa zina shughuli za kisekta zinazotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zipo chini ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI, hivyo tumeona ni muhimu tukakutana ili kupata namna bora ya kuratibu utekelezaji wa shughuli hizo,” alisema Cheyo.

Kikao kazi hicho cha siku moja ambacho ni mwendelezo wa kikao kilichofanyika mwaka wa fedha 2023/24, kimeudhuriwa na wakurugenzi wa sera na mipango kutoka wizara za kisekta na taasisi zake pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI.