TATIZO la shinikizo la damu likiambatana na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza, yanaongezeka kwa kasi kubwa na kuwa tishio duniani kiuchumi na kijamii hasa kwenye sekta ya afya.
Uchumi hutegemea rasilimali watu lakini magonjwa haya yamekuwa sababu kubwa ya kupunguza nguvu kazi kupitia majanga yanayosababishwa nayo. Tatizo hili linaonekana kuongezeka kwa kasi kubwa zaidi katika siku hizi na zijazo kwenye nchi zenye uchumi wa chini na kati.
Hii huashiria kwa namna gani Tanzania iko kwenye kundi hili kubwa kati ya nchi zinazopitia madhara haya ya magonjwa yasiyoambukizwa.
Kwa bahati nzuri, Rais Samia Suluhu Hassan kushirikiana na viongozi wenzake kitaifa, anajitahidi kuboresha afya katika nchi nzima ili kupambana na mambo yaliyo tishio kwa afya, yakiwamo magonjwa hayo.
Pamoja na jitihada hizo, kasi ya magonjwa yasiyoambukiza imekuwa ikiongezaka kila mwaka, hivyo kurudisha nyuma jitihada za Rais Samia na serikali yake katika kuboresha sekta ya afya.
Kupitia jarida la Global Health, utafiti uliofanyika nchini, uliochapishwa Novemba, 2023 kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, unaonesha kwamba Tanzania ni moja ya nchi inayokumbwa na janga la ukuaji mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza.
Magonjwa makubwa manne yanaoyongoza kwenye magonjwa yasioambukiza ni maradhi ya moyo, saratani, mfumo wa upumuaji na sukari. Magonjwa haya yanachangia kwa asilimia 40 kwenye magonjwa yasiyoambukiza.
Katika kundi hili, magonjwa haya yanaonekana dhahiri kwamba shinikizo la damu na sukari yanaongoza kwani yanachukua asilimia 25.9 na 9.1 mtawalia. Magonjwa hayo yanaendelea kuwa sehemu moja ya tatu ya vifo vyote vinatokana na magonjwa ya kutokuambukiza.
Awali shinikizo la damu na sukari yalionekana na yaliaminika kuwa yanawapata watu wenye umuri mkubwa, yaani wazee, lakini kwa sasa mambo yamebadilika kwa kuwa yanawapata hata watoto. Sababu kubwa inayochangia ongezeko la magonjwa hayo ni mabadiliko ya kimaisha unaoendelea duniani na uigaji wa namna ya kuishi tofasuti na awali.
Shinikizo la damu ni tatizo ambalo linatakiwa kupewa umuhumi katika mapambano ili kuepusha kuenea zaidi na kugharimu Maisha ya watu. Njia mojawapo ni kudhibiti shinikilo za damu bila kutumia dawa. Njia hizo ni pamoja na;-
Kupuguza uzito
Tatizo la shinikizo la damu limeonekana likiendana sana na uzito mkubwa, hivyo njia mojawapo inayotakiwa katika kudhibiti ni kupungua uzito kwa alama moja au mbili ya mmhg ya kwenye kifaa cha kupimia shinikizo la damu.
Pia ubukwa wa kiuno ni muhimu pia sababu kuwa na uzito mkubwa kiunoni imeonekana ikiendana na ongezeko la kiwango cha shinikizo la damu. Wanaume wanatakiwa wasizidi mzunguko wa sentimita 102 na wanawake 89.
Fanya Mazoezi
Inashauriwa mtu kufanya mazoezi mara kwa mara angalau dakika 30 kwa siku na mara tano kwa wiki. Mazoezi yanayotakiwa ni ya kawaida yenye kutoa jasho ikiwamo kutembea, kukimbia, kuruka kamba na kucheza.
Chakula Bora
Chakula bora ni chenye matunda, mbegu, mboga za majani na kisicho na mafuta mgando mengi yaani lehemu nyingi ambayo huenda kugandia kwenye mishipa ya damu na kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu maradufu.
Matumizi ya Chumvi
Inashauriwa kuwa kwa siku matumizi ya chumvi yasizido kiwango cha miligirami 1500 na kuepuka kuongeza kwenye chakula chumvi wakati kikiwa mezani, yaani chumvi mbichi.
Acha/punguza Pombe
Acha kutumia pombe. Ili kuepusha tamaa ya kunywa pombe nyingi, inashauriwa kutumia kiwango kidogo ambacho kinaweza kutokuwa na madhara mwilini, yaani bilauri mbili kwa wanaume na moja kwa wanawake kwa siku.
Acha Kuvuta Sigara
Sigara huchangia kuharibu mishipa ya damu na hata kuharibu mapafu ambayo husaidia pia kwenye zuio la shinikizo la damu.
Panga Muda wa Kulala
Kulala vizuri na kwa muda wa kutosha husaidia kupunguza matatizo ya shinikizo la damu. Pia kufanya mwili kujiponyesha pale ulipoharibika.
Punguza Mawazo
Imeonekana watu wenye msongo wa mawazo wa muda mrefu, mfano watu waliofiwa au matatizo ya uhusiano ambao hawakuwa na shinikizo la damu mwanzo, huanza kupata tatizo hilo.
Angalia Msukumo wa Damu
Inashauri kuwa mtu anatakiwa mara kwa mara kuangalia msukumo wa damu nyumbani au hosipitalini. Uangalizi wa afya wa mara kwa mara, husaidia kwa kiasi kikubwa ugunduzi wa magonjwa mbalimbali mapema na kuzuia au kutibu pale inapotakiwa.
Msaada wa Familia
Watu wa familia husaidia ufuatiliaji wa afya yako vizuri na hata kukumbusha kutumia dawa vizuri.
Haya yote yakifatwa na kufanyika vizuri yatasaidia sana kwenye tatizo hilo. Hizi ni njia za awali kwa wagonjwa wa shinikizo la damu. Kwa mgonjwa wa shinikizo la damu, wanatakiwa kuhudhuria kiliniki na kufuata ushauri wa daktari ikiwamo kutokuacha matumizi ya dawa.
• Dk. Mabula Budodi ni daktari wa binadamu na anapatikana kwa namba 0710 980096 na baruapepe [email protected]
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED