Kamati Bunge zashauri ufungwaji CCTV mradi SGR kudhibiti uhalifu

By James Kandoya , Nipashe Jumapili
Published at 10:22 AM Nov 10 2024
Kamati Bunge zashauri ufungwaji CCTV mradi SGR kudhibiti uhalifu
Picha:Mtandao
Kamati Bunge zashauri ufungwaji CCTV mradi SGR kudhibiti uhalifu

KAMATI za Kudumu za Bunge ya Bajeti na Miundombinu zimelishauri Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuweka mifumo ya ulinzi wa miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiwamo ufungaji wa kamera za CCTV.

Kwa mujibu wa kamati hizo, lengo ni ili kudhibiti uharibifu wa miundombinu ya nyaya za umeme unaofanywa na watu wasio na nia njema na mradi huo.

Ushauri huo ulitolewa jana hivi karibuni kuripotiwa kusimama kwa treni mpya ya mwendokasi, huku sababu zilizobainishwa ikiwa ni uharibifu wa miundombinu ya nyaya za umeme.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, baada ya kikao kazi kilichokutanisha pia, Kamati ya Kudumu ya Bajeti, serikali pamoja na uongozi wa shirika hilo kujadili mipango na mwelekeo wa huduma za usafiri.

 Kakoso alisema kamati imebaini kuna upungufu na kasoro za kiulinzi katika baadhi ya maeneo.

Alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo iliyokwisha na inayoendelea hivyo si vyema ikaachwa bila ulinzi.

“Watu wasio na nia njema na nchi yetu wameanza kukata miundombinu ya nyaya za umeme na kusababisha kusimama kwa huduma maeneo fulani fulani,” alisema Kakoso.

Alisema mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa una faida nyingi kwa nchi na mwananchi mmoja mmoja endapo kama itasimamiwa na kutunzwa vyema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Oran Njeza, alisema Tanzania itakuwa na uchumi mzuri kuliko nchi nyingine yoyote iwapo ujenzi wa reli hiyo utakamalika.

“Maono ya TRC ni kutoa huduma bora na za uhakika, hivyo haitaweza kufanikiwa iwapo kuna watu wachache wana hujumu miundombinu hii,” alisema.

Njeza aliishauri serikali kuhakikisha reli hiyo inawaunganisha na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zina uhitaji wa miundombinu ya njia ya reli ili kufika na kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye, alisema amepokea maagizo yote ya kamati hizo na kuahidi kuyafikisha kwa waziri mwenye dhamana kwa ajili ya utekelezaji.

“Tumepokea maelekezo ya kamati hizi tutashirikiana na Bunge kuhakikisha haya yote yanatekelezwa,” aliahidi.

Akitoa ufafanuzi kukwama kwa treni ya mwendokasi ya Mchongoko siku moja baada ya uzinduzi wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alibainisha kuwapo kwa njama za ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya watu ambao sio waaminifu.

“Tutachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kuhusika kuhujumu miundombinu yetu ya reli,” alisema Kadogosa.