JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia dereva wa bodaboda, Juma Afyusisye (38), mkazi wa Iwambi mkoani humo kwa tuhuma za kummwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto mtoto (jina linahifadhiwa) kisa Sh. 10,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Benjamin Kuzaga, alisema tukio hilo lilitokea Jumanne wiki hii.
“Sababu za tukio hilo ni baada ya mtuhumiwa kumpa mtoto huyo Sh. 10,000 akanunue maandazi ya Sh. 5,000 dukani, lakini mtoto akatumia fedha hiyo kwa matumizi yake, hakurudi na hiyo fedha,” alisema Kamanda Kuzaga.
Alisema mtoto huyo wa kiume ambaye ni mwanafunzi darasa la pili katika Shule ya Msingi Iwambi, amejeruhiwa maeneo mbalimbali mwilini.
Alisema baada ya mtoto huyo kurudi nyumbani akiwa hana fedha wala maandazi aliyotumwa, mtuhumiwa alijichukulia sheria mkononi kwa kummwagia petroli kwenye shati alilovaa kisha kuwasha kiberiti.
“Mtoto amelazwa Hospitali Teule ya Ifisi katika Mji Mdogo wa Mbalizi akiendelea kupatiwa matibabu. Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wazazi au walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, badala yake watafute njia sahihi ya kuwaadhibu watoto pindi wanapokosea,” alishauri.
Hata hivyo, Kamanda Kuzaga alisema Jeshi la Polisi halitavumilia wala kufumbia macho vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii, litaendelea kuchukua hatua kali kwa watuhumiwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza akiwa hospitalini, mtoto huyo alisema, alipewa Sh. 10,000 kwenda dukani kununua maandazi na sukari na wakati akirejea nyumbani alipoteza Sh. 200, ndipo mtuhumiwa huyo akakasirika na kuchukua tairi na kumwagia mafuta ya petroli na kuwasha moto kisha kuondoka.
"Mjomba Inno alivyoniona akaenda kuwaita watoto wenzake na kunimwagia maji ili kuzima moto, lakini haukuzima alichukua mchanga kunimwagia ukazima. “Nilisikia sauti za dereva akisema ‘hawa watoto wasije wakaleta umbea’ akamwita bosi wake akanichukua na kunipeleka zahanati,” alisimulia mtoto huyo.
Mama wa mtoto huyo, Marita Abiud alisema, alipigiwa simu na wasamaria wakimweleza kuhusu tukio hilo na alipofika nyumbani alipata taarifa kwamba, aliyefanya kitendo hicho ni jirani yake, ndipo alipokwenda zahanati na kumkuta mtoto akiwa katika hali mbaya na kumpeleka hospitalini.
Baba wa mtoto huyo, Uswege Mwambigila, ameonesha kushangazwa na kitendo cha mtuhumiwa huyo kumchoma moto mtoto wake na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali hasa eneo la kitovu.
“Amemwagia mwanangu petroli sijui lengo lake lilikuwa ni nini au alikuwa na nia ya kumuua. Kama ni madai hajarudisha chenji, alipaswa kuja kwa wazazi ili tumlipe, yawezekana alikuwa na lengo la kumuua mtoto wangu,” alidai Mwambigija.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED