RIPOTI MAALUM: Hatari watoto kubebwa 'mshikaki' kwenye bodaboda

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:42 AM Dec 08 2024
Dereva wa pikipiki maarufu bodaboda, akiwa amebeba wanafunzi wanne, mtindo maarufu kama mshikaki, kitendo
ambacho ni hatari kwa usalama barabarani.
Picha:Mtandao
Dereva wa pikipiki maarufu bodaboda, akiwa amebeba wanafunzi wanne, mtindo maarufu kama mshikaki, kitendo ambacho ni hatari kwa usalama barabarani.

TAZAMA ulimwengu wanafunzi wanaobebwa kwenye bodaboda kwa mtindo wa mishikaki kuwahi shuleni. Huu ni utaratibu wa muda mrefu ambao sasa umechukuliwa kama wa kawaida, huku baadhi wakiishia kupata majeraha na wengine kuwa katika hatari ya kupoteza maisha.

Akiwa na miaka saba, mtoto wa  Alex Simon, mkazi wa Mtaa wa Wigehe, Kata ya Zongomela, Kahama mkoani  Shinyanga, wakati akirejea nyumbani akitoka shuleni, akiwa kwenye pikipiki aliunguzwa na bomba la kutolea moshi (exhaust). 

Anasema licha ya mtoto huyo kupiga kelele kutokana na maumivu ya moto,  dereva aliyembeba hakusikia kutokana na upepo mkali na  kofia ngumu aliyokuwa amevaa hadi walipofika nyumbani.

 “Nilitumia gharama kubwa kumtibu mtoto. Alikosa  masomo kwa mwezi mzima. Binafsi siwezi kurudia tena kutumia usafiri huu wa pikipiki kumpakia mtoto wangu,” anasema Simon.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhan Ng’anzi, anasema licha ya kutokuwapo kwa ripoti za hivi karibuni zinazohusu matukio ya ajali za watoto wanaobebwa katika pikipiki, ni kosa kisheria kubeba abiria zaidi ya mmoja katika vyombo hivyo na pia, kumbeba mtoto mwenye umri chini ya miaka tisa.

SHERIA

Kanuni za usafirishaji kwa njia ya bajaji na pikipiki ya mwaka 2010 zilizofanyiwa marejeo mwaka 2017, zilizotungwa kupitia Sheria ya Utoaji Leseni za Usafirishaji ya Mwaka 2010, kanuni namba 14 (2) imepiga marufuku mtoto mwenye umri wa chini ya miaka tisa asibebwe kwenye pikipiki peke yake kama abiria.

Sheria ya Barabarani Kifungu cha 168 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, kuhusu Sheria za Abiria anayetumia mabasi, daladala, teksi na pikipiki, imepiga marufuku kupanda pikipiki ambayo tayari imebeba abiria.

Kadhalika, imezuia mtoto mdogo kukaa mbele ya pikipiki au gari pamoja na mtu yeyote aliyebeba mtoto mdogo kukaa mbele.

Sheria hiyo pia imepiga marufuku kubeba zaidi ya abiria mmoja, ikishauri waendesha pikipiki au skuta pamoja na abiria wake, lazima wavae kofia ngumu  iliyothibitishwa ambayo imefungwa kiusalama.

Pia imemtaka abiria wa kiti cha nyuma kukaa kwa kutanua miguu kwenye kiti halisi na kuweka miguu yote miwili kwenye sehemu ya kukanyagia.

Ukiukwaji wa sheria na kanuni hizo, mhusika anayekamatwa na kutiwa hatiani, atatozwa faini na kuzuiwa kuendesha na anaweza kupelekwa jela kwa miaka hadi mitano.

WANANCHI

Mmoja wa wananchi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, akiwamo mkazi wa Kata ya Nyasubi, Emmanuela Gwamagobe, anasema alfajiri na jioni wanafunzi hupakiwa kwenye pikipiki wakiwa wanne au zaidi.

Kutokana na hali hiyo, Gwamagobe anakishauri kitengo cha usalama barabarani kuwachukulia hatua madereva pikipiki wanaobeba wanafunzi kwa mtindo wa ‘mishikaki’ ambao huhatarisha maisha yao.

Anashauri wanaokutwa na makosa hayo walipishwe fani ya Sh. 30,000 badala ya Sh. 10,000 ya sasa na kuwabana wazazi ambao watoto wao wamepakiwa  mtindo wa mishikaki kwenye bodaboda.

 Mkazi wa Sengerema, mkoani Mwanza, Eugenia Lameck, anasema wakati mwingine watoto wanapakiwa kwenye vyombo hivyo, huku wanakokwenda ni karibu.

Mkazi wa Majengo, wilayani Magu, Godfrey Kweka, anasema kinachosababisha wazazi kuwapakia watoto wao kwenye pikipiki ni kurahisisha usafiri.

“Ukimwacha mtoto aende kupanda daladala analazimika kuamka saa 11 alfajiri na kufika shuleni saa tatu hadi saa nne asubuhi,” anasema.

KAULI ZA BODABODA

Mwendesha bodaboda mkazi wa Mtaa wa Majengo, Magu, Jotham Kennedy, anasema sababu kubwa ya wazazi wanaowapa bodaboda watoto wao ili kuwapeleka shuleni na kuwarejesha nyumbani ni kutokana na kutokuwa na uwezo wa kugharamia magari ya shule na kukwepa usafiri wa umma kuepuka watoto wao kuchelewa shuleni.

Kennedy anasema kupitia kazi hiyo, wazazi wanawalipa kwa mwezi lengo likiwa ni kupunguza hatari ya mtoto kupotea kutokana na watoto wao kuwa wadogo.

Anasema huwalazimu kubeba watoto wengi katika pikipiki ili kuwasaidia kuongeza pato la mwisho wa mwezi.

“Ili kuingia makubaliano ni lazima awe anakufahamu vizuri. Mtoto mmoja kumpeleka na kumrudisha kwa kila siku ni Sh. 2,000 na kwa shule zilizoko karibu, wakiwa wawili ni sawa na Sh.4,000.

“Lakini mnaweza kufanya maelewano ukabeba Watoto wawili kwa Sh.3,000 kwa siku, hivyo unakuwa na uhakika wa Sh. 90,000 kwa mwezi. Ukiongeza  watoto wengine wawili wa mzazi mwingine, inakuwa Sh. 180,000 hivyo inatusaidia kumaliza majukumu muhimu nyumbani,” anasema Kennedy.

Anasema usafiri huo ni salama na unasaidia kumwepusha mtoto na vitendo vya ukatili njiani lakini tatizo lililoko ni kwa baadhi ya bodaboda kutokuzingatia sheria na usalama wa mtoto, hivyo kuhatarisha maisha yao kwa asilimia kubwa.

CHANZO CHATAJWA

Baadhi ya wazazi ambao watoto wao hubebwa katika pikipiki hizo, wanataja ugumu wa maisha kama chanzo cha wao kuruhusu watoto wao kubebwa katika usafiri huo wa pikipiki.

Mzazi na mkazi wa Sengerema, mkoani Mwanza, Peter Marco, anasema analazimika kuwapakiza watoto wake katika pikipiki moja kutokana na uwezo wa kifedha wa kumudu kuwalipia usafiri wa gari kuwa mdogo.

Anasema wazazi wamekuwa wakiungana ili Watoto wao wabebwe kwenye pikipiki moja kuepuka gharama.

Marco anasema kwa wastani kwa watoto wawili, hubebwa kwa gharama ya Sh. 3,000 (kwenda na kurudi nyumbani) kila siku.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia shule moja ya mchepuo wa Kiingereza mkoani Mwanza, imeonesha  kwa miezi mitatu kwa mtoto anayetumia basi la shule ni Sh. 100,000 ambapo kwa usafiri wa pikipiki anachokwepa ni Sh. 10,000.

Fomu ya shule hiyo imebainisha kuwa kwa kila miezi mitatu mzazi atalipa fedha za usafiri Sh.100,000 na kuwa kwa vipindi vyote vine, mzazi atalipa Sh.400,000 ambako kwa wastani wa watoto wawili wanaobebwa katika pikipiki moja wanalipa Sh.3,000, sawa na Sh. 1500 kwa mtoto mmoja.

Kwa maana hiyo, mtoto anayetumia pikipiki kwa mwezi hutumia Sh. 30,000 na kwa miezi mitatu ni Sh. 90,000, tofauti ikiwa ni Sh.10,000 kulinganisha na mtoto anayetumia usafiri wa basi la shule.

Mzazi mwingine na mkazi wa Sengerema, Jenifer Christopher, maarufu kama Mama Petu, anasema anapoingia makubaliano na mtu wa pikipiki ili kumbeba mtoto wake, hafahamu kama mtu huyo ana makubaliano kama hayo sehemu nyingine.

“Shida ni kwamba, yule unayemwamini, kuna mzazi mwingine naye anamwamini, siwezi kumkatazamtu wa pikipiki kumbeba mtoto wa mwingine, ana haki ya kuwahi shuleni. Ninachowaomba bodaboda ni kuwa makini huko barabarani ili kuepusha ajali,” anasema.

WADAU WANENA

Baadhi ya wadau wa elimu akiwamo, Diwani wa Kinamapula, Sharifu Samweli, anasema ubebaji wa abiria zaidi ya wawili katika pikipiki ni uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.

Anasema wazazi wanaokodisha pikipiki ili kubeba watoto wao wanapokwenda shuleni na kurejea nyumbani hasa ni wale kutoka katika shule binafasi.  Anasema katika kuondokana na tatizo hilo ni vema Jeshi la Polisi likashirikisha viongozi wa vyama vya waendesha pikipiki na bajaji kukabiliana ubebaji usiozingatia sheria.

Meneja wa Shule ya Sekondari Rwepa’s, Frank Samweli, anakiri baadhi ya shule binafsi, wazazi wengi wamekuwa wakiwapeleka watoto wao kwa kutumia usafiri wa pikipiki na bajaji, wakiwa wamekaa zaidi ya wawili.

Samweli alishauri wazazi pamoja na madereva wanaochochea kuvunjwaji wa sheria za usalama barabarani, kuwajibishwa kisheria.

KAULI YA POLISI

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabara Wilaya ya Kahama, Mrakibu Msaidizi (ASP) Flora Nangawe, anasema amefanya utafiti wake na kubaini wazazi na walezi wanaungana kukodisha pikipiki moja na kubeba watoto wao, jambo ambalo ni hatari.

Nangawe anasema wamejipanga kuchukua hatua za kisheria kwa dereva pikipiki atakayebainika amebeba wanafunzi kwa mtindo wa mishikaki, atatozwa faini ya Sh. 10,000 na makosa yanapojirudia atafutiwa leseni yake na mzazi atawajibishwa kisheria.

 Askari wa usalama barabarani, Sajenti Mswadiku Kempantu, anasema mara kwa mara hutoa elimu kuhusu changamoto hiyo, lakini baadhi hukaidi na wanapokamatwa hutozwa faini na wakati mwingine hunyang'anywa pikipiki kwa muda ili wajirekebishe.

Mswadiku anasema pia, hairuhusiwi mtoto chini ya miaka tisa kubebwa na bodaboda kwa kukaa mbele kwenye tanki la mafuta.

KANUNI YAJA

DCP Ng’anzi, akizungumza na Nipashe, anasema licha ya kutokuwa na ripoti za hivi karibuni zinazohusu matukio ya ajali za watoto, lakini anakiri hilo ni kosa kisheria.

Anabainisha kwamba ni kosa si kwa dereva wa pikipiki kubeba abiria zaidi ya mmoja na pia kubeba mtoto mwenye umri wa chini ya miaka tisa katika vyombo hivyo.

Anasema operesheni ya kukamata madereva pikipiki wanaokiuka sheria hiyo inaendelea katika vituo vyote vya polisi nchini.

“Tumeliona tatizo hilo na tunaendelea kulidhibiti, wito wangu kwa wazazi na walezi waache tabia ya kuruhusu watoto wao kubebwa katika pikipiki chini ya miaka tisa.

“Watoto kama ni wakubwa, abebwe mmoja. Tutawakamata wote wanaobeba abiria zaidi ya mmoja, kwani huo ni ukiukwaji wa sheria, hatutowafumbia macho, kila mara tunatoa elimu kuhusu suala hiya,” alisema Ng’anzi.

Kuhusu sheria dhidi ya wazazi wanaoruhusu watoto wadogo kubebwa katika pikipiki na wakati mwingine zaidi ya mmoja, Ng’anzi anafafanua kwamba, sheria iliyoko haimuweki hatiani mzazi.

Anasema kutokana na changamoto hiyo, wanatazama namna ya kuweka kanuni zitakazombana na mzazi moja kwa moja ili kuleta fundisho kwa wengine.

Hata hivyo, Ng’azi anasema kwa kuwa sheria inamzungumzia mwenye pikipiki, wataendelea kushughulika nao kwa sababu wanajua kanuni za uendeshaji barabarani na wanazikiuka kwa kujua.

Imeandaliwa na Vitus Audax (MWANZA), Neema Emmanuel (MWANZA), Shaban Njia(KAHAMA), Elizabeth Seleman (SENGEREMA)