Rais Samia abana vigogo wizara nne

By Neema Hussein , Nipashe Jumapili
Published at 02:03 PM Jul 14 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan.

VIGOGO katika wizara nne wamewekwa 'kitanzini' Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza wizara zao zikamilishe miradi zinayotekeleza ili kutoa huduma kwa wananchi.

Ameagiza Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) kuhakikisha hadi mwezi Septemba mwaka huu, mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea umeme wa Sh. bilioni 48 na ule wa njia ya kupitisha umeme kwenda Gridi ya Taifa kutoka Tabora hadi Katavi unaogharimu Sh. bilioni 116 inakamilika.

Pia ameagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha barabara zote zinazojengwa zikamilike kwa haraka na zile zinazotakiwa kuanza utekelezaji zifanyiwe kazi haraka.

Rais Samia alitoa maagizo hayo jana wakati akihutubia wananchi wa  Wilaya ya Mlele, mkoani hapa, akielekeza mradi huo wa umeme ukamilike ndani ya muda huo ili wananchi  wapate umeme wa uhakika.

Pia aliagiza Wizara ya Habari na Mawasiliano kuimarisha mawasiliano katika maeneo mkoa huo kwa kuwa wananchi wasipopata taarifa sahihi hawawezi kupata uelewa kuhusu serikali yao na yanayofanywa na serikali hiyo.

Katika ziara hiyo, Rais Samia jana alitembelea na kukagua miradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea umeme wa Gridi ya Taifa cha Mlele kutoka Tabora hadi Katavi ambao umefikia asilimia 97 ya ujenzi wake.

Alisema mradi huo utakapokamilika utakuwa suluhisho la kukatikatika kwa umeme katika mkoa huo.

"Tangu nchi ipate uhuru, mkoa huu ulikuwa haujaunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa, gharama zinazotumika katika kuzalisha umeme kwa kutumia jenereta ni kubwa kwani kila mwezi mkoa huo unatumia zaidi ya Sh. bilioni mbili katika kuzalisha umeme unaosambazwa kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi.

"Nipo hapa Katavi kwa ziara ya kikazi na kichama, nikiwa hapa nitatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa, na asubuhi nimekagua kituo cha kupokea umeme Gridi ya Taifa kilichopo hapa Mlele.

"Nimeona kazi nzuri inayofanyika, hii tunatekeleza Ilani cha Uhaguzi ambayo tuliahidi kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi," alisema.

Rais Samia  aliomba wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazotokana na kupata umeme wa Gridi ya Taifa na kulipia gharama za umeme kutokana na matumizi wanayotumia.

Mkuu wa Nchi pia alishukuru wananchi waliotoa maeneo yao kupisha mradi ambao wanasubiri kulipwa fidia na kusisitiza kuwa watu wote ambao wamepitiwa na mradi watalipwa fedha zao zote kwa kuwa kuna Sh. bilioni nne zilizotengwa kwa ajili yao.

Rais Samia alisema Wizara ya Ujenzi imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara ambapo barabara kutoka Tabora hadi Katavi imekamilika kwa kiwango cha lami.

Alisema serikali inatarajia kuanza ujenzi wa barabara ya Kibaoni-Makutano ya Mlele ambayo ni kilomita 50, Vikongwe-Uhavywe kilomita 25, Luhavywe-Mishamo zaidi ya kilomita 37 na Kakwira-Kalema kilomita 110 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami na fedha zipo.

"Nimefurahishwa na kazi inayofanywa na Wizara ya Ujenzi kwani barabara kutoka Tabora- Mpanda ni mkeka tu, nimepita mpaka nikasinzia, haya ni maendeleo makubwa sana.

"Pamoja na hayo serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, tunataka mkoa huu tuunganishe kwa lami maeneo yote ili kurahisisha ukuaji uchumi wa mkoa huu.

"Ninaagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha barabara zote zinazojengwa zikamilike haraka na zile ambazo zinatakiwa kuanza utekelezaji wake mzifanyie kazi haraka ili mkoa huu uunganishwe na lami pande zote," aliagiza.

Rais Samia pia alisema amepokea maombi ya Mbunge wa Katavi, Issack Kamwelwe, kuhusu wananchi wa jimbo hilo kupewa maeneo ya kulima na kufuga katika Hifadhi ya Taifa Katavi.

"Nimepokea maombi ya mbunge wenu na yatafanyiwa kazi na bahati nzuri Waziri wa Maliasili yupo hapa. Ninachoomba wananchi wa mkoa huu na nchi nzima kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira.

"Tunafahamu kuna uhaba wa ardhi kulingana na idadi ya watu. Watu wa mkoa huu mmebarikiwa kuzaa, lakini uhaba wa ardhi usiwe chanzo cha kuharibu mazingira ya hifadhi zetu.

"Kinachotakiwa ni kukaa na serikali na kuangalia mahitaji ya watu, basi tunachukua hatua ya kukata eneo la hifadhi ili wafanye shughuli za kilimo na ufugaji," alisema.

Alionya viongozi wasihamasishe wananchi kuvunja sheria, baadaye kuwa mstari wa mbele kutetea wanaochukuliwa hatua kutonana na uvunjaji sheria.

Alisema serikali itajenga minara ili usikivu wa  vyombo vya habari uwe rahisi kwa kuwa "jamii yenye taarifa ndiyo inaweza kufanya uamuzi sahihi".