Mkandarasi mradi maji aingia mitini

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 03:16 PM Feb 11 2024
kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
PICHA :Na Mtandao
kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

MRADI wa uchimbaji visima 11 unaogharimu Sh.milioni 363.3 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida umekwama baada ya mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo kukimbia, huku akiwa ameshalipwa Sh.milioni 73.

"Mkandarasi huyu kila tukimpigia simu aje kwenye kikao haji na hajaonekana 'site' tangu Novemba 2023 na kimsingi Sh.milioni 73 alizolipwa ambazo zinatolewa na Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ambao upo chini ya Wizara ya Maji hazilingani na kazi aliyoifanya,” amesema Kaimu Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Bernard Marcely.

Hayo yamebainika wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni baada ya Kaimu Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Bernard Marcely akijibu maswali ya madiwani.

Madiwani hao walihoji kutokamilika kwa miradi ya kuchimba visima kwenye kata zao.

Marcely alisema kulingana na mkataba Kampuni ya Coyesa Co.Ltd ilipewa zabuni ya kuchimba visima 11 wilayani Manyoni kwa gharama ya Sh.milioni 363.3 kazi ambayo ilitakiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Alisema mkandarasi huyo tangu apewe kazi hiyo na kulipwa Sh.milioni 73 amechimba visima vitano ambavyo vinatoa maji katika vijiji vya Mbwasa, Majiri, Igwamalete na Makasuku ambapo baada ya hapo ameingia mitini na hajulikani alipo.

"Mkandarasi huyu kila tukimpigia simu aje kwenye kikao haji na hajaonekana 'site' tangu Novemba 2023 na kimsingi Sh.milioni 73 alizolipwa ambazo zinatolewa na Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ambao upo chini ya Wizara ya Maji hazilingani na kazi aliyoifanya,” alisema.

Marcely alisema kutokana na ukaidi wa mkandarasi huyo RUWASA imeanza mchakato wa kuvunja mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine ambaye atafanya kazi ya kuchimba visima sita vilivyobaki.

Baada ya maelezo hayo, madiwani waliitaka RUWASA kuvielekeza Vyombo vya Utoaji Huduma ya  Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya maji kwa jamii.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mlagaza, alisema endapo CBWSOs hazitajenga utamaduni wa kutoa taarifa ya mapato na matumizi basi miradi ya maji inaweza kufa kutokana na usimamizi na matumizi mabaya ya fedha za maji.

Hata hivyo, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Marcely alisema baadhi ya CBWSOs hazifuati maelekezo lakini ofisi ya RUWASA inaendelea kuwaelekeza na kuwajengea uwezo viongozi wa vyombo hivyo ili viweze kufuata sheria na kanuni zilizotolewa na RUWASA.