MATOKEO KIDATO VI, UALIMU: Udanganyifu wapungua, Hisabati bado maumivu

By Rahma Suleiman , Nipashe Jumapili
Published at 02:22 PM Jul 14 2024
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Ali Mohamed.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Ali Mohamed.

BARAZA la Mitihani (NECTA) limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka huu, ufaulu ukiongezeka hadi wastani wa asilimia 90 kwa masomo yote isipokuwa somo la Hisabati ambalo ufaulu wake ni wa asilimia 78.

Hata hivyo, ufaulu wa somo la Hisabati umeongozeka kulinganishwa na mwaka jana ambao ulikuwa wa asilimia 68. Ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 99.92.

Akitangaza matokeo hayo jana visiwani Banzibar, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Ali Mohamed,  alisema wasichana wanaongoza; waliofaulu ni 49,837 sawa na asilimia 99.61 kulinganishwa na wavulana 61,219 (asilimia 99.28).

Alisema watahiniwa wote wa shule na kujitegemea waliofanya mtihani huo walikuwa ni 111,056.

"Kwa mwaka 2023, watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 104,549 sawa na asilimia 99.23, hivyo ufaulu wa jumla kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 0.20 kulinganishwa na mwaka 2023," alisema.

Dk. Mohamed alisema ubora wa ufaulu kwa kuzingatia madaraja kwa watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 102,719 sawa na asilimia 99.4 wamepata ufaulu mzuri wa madaraja ya kwanza hadi la tatu.

Alisema watahiniwa wengi wapo katika ufaulu wa daraja la kwanza na la pili ambapo daraja la kwanza ni watahiniwa 47,862 sawa na asilimia 46.32 na daraja la pili ni 42,359 sawa na asilimia 40.99.

Katibu huyo alisema kuwa mwaka jana watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja ya kwanza hadi la tatu walikuwa 95,442 sawa na asilimia 99.30, hivyo ubora wa ufaulu kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 0.1 kulinganishwa na mwaka jana.

Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 103,252 sawa na asilimia 99.92 ya watahiniwa wenye matokeo, ambapo wanawake ni 46,615 sawa na asilimia 99.93 na wavulana 56,637 sawa na asilimia 99.91 na watahiniwa walioshindwa mitihani kwa sababu mbalimbali ikiwamo za kiafya ni 84 sawa na asilimia 0.08.

"Mwaka 2023 watahiniwa 96,010 sawa na asilimia 99.90 ya watahiniwa wa shule walifaulu mtihani huo, hivyo ufaulu wa watahiniwa wa shule umeongezeka kwa asilimia 0.02 kulinganishwa na mwaka jana," alisema.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, Dk. Muhamed alisema waliofaulu ni 7,804 sawa na asilimia 93.34 ambapo mwaka jana walikuwa 8,539 sawa na asilimia 92.30.

Alisema ufaulu wa watahiniwa hao kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 1.04.

Kuhusu ubora wa ufaulu, Dk. Mohamed alisema kwa kuzingatia madaraja waliopata watahiniwa wa shule, unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 102,719 sawa na asilimia 99.40, wamepata ufaulu mzuri wa madaraja ya kwanza hadi tatu.

MATOKEO YALIYOFUTWA

Dk. Mohamed alisema baraza hilo limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 326 kati yao, 304 ni kidato cha sita na 12 ya ualimu.

Alisema matokeo hayo yamezuiwa kutokana na matatizo ya kiafya ambapo walipata matatizo na kushindwa kufanya mitihani na watahiniwa hao wamepewa fursa kufanya mitihani yao mwaka 2025.

Kuhusu matokeo yaliofutwa, Katibu  Mtendaji huyo alisema watahiniwa 24 wakiwamo 22 wa kidato cha sita wamefutiwa matokeo yao. Kati ya hao, 17 wa shule na watano wa kujitegemea na wawili kwa ngazi ya ualimu ambao walibainika kufanya udanganyifu.

Alisema udanganyifu uliofanyika kwa watahiniwa hao ni pamoja na kuingia na simu katika chumba cha mitihani, kusaidiana kwa kupeana majibu na waliokutwa na notsi.

Dk. Mohamed alipongeza watahiniwa wote kwa kuwa na utulivu na kuzingatia taratibu za mitihani katika kipindi chote cha uendeshaji mitihani pamoja na kamati za uendeshaji mitihani za mikoa, wakuu wa shule, wasimamizi na wasahihishaji mitihani hiyo.

Alisema licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza zikiwamo za mafuriko yaliyotokana na mvua na baadhi ya shule kuharibika kwa miundombinu pamoja na kimbunga Hidaya, wanafunzi walisoma kwa bidii na kufanikiwa kufaulu vizuri.