Wizara ya Kilimo, inatarajia kupeleka sampuli za udongo wa halmashauri nane za Mkoa wa Pwani maabara, ili kubaini aina ya mazao yanayostawi na kubatilisha matumizi ya maeneo yasiyofaa kwa kilimo kwa shughuli nyingine.
Kwa mujibu wa kiongozi wa timu ya uchunguzi huo, Ofisa Kilimo wa wizara hiyo, Miriam Chanzi, sampuli hizo zimechukuliwa katika Halmahauri ya Wilaya ya Kibaha, Bagamoyo, Chalinze, Kisarawe, Kibiti, Mkuranga, Rufiji na Mafia.
Miriamu, amesema wamechimba mashimo madogo 2,375 na kuchukua sampuli 4,732 na kwa mashimo makubwa 241 sampuli 733.
Akizungumzia umuhimu wa upimaji wa afya ya udongo, alisema ni kiungo muhimu kuendeleza sekta ya kilimo kutoa mwongozo wa aina ya mazao yanapaswa kulimwa na mbolea ya kutumia katika halmashauri hizo na nyingine nchini.
Ameitaka jamii kulipokea zoezi la upimaji wa afya ya udongo kwa ushirikiano, ili wizara hiyo ikamilishe kwa mikoa iliobaki ya Tanzania Bara na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo nchini.
Amesema uchukuaji huo wa sampuli hizo uliambatana na ukusanyaji wa taarifa za kijamii kwa lengo la kuiwezesha wizara kupata takwimu sahihi zajamii inayopimiwa udongo wake na kuoanisha matokeo yatakayopatikana maabara.
Ameeleza vilevile ina lengo la kuwa na uhalisia wa taarifa zilizopatikana katika jamii kusaidia kufanya maamuzi juu ya namna bora ya kuleta maendeleo ya sekta ya kilimo kwa eneo husika.
Pwani ni kati ya mikoa inayofanya vizuri kwenye sekta ya viwanda kutokana na wingi wake na fursa za kutumia mazao ya kilimo kama malighafi ya viwandani.
Upimaji huo, pia una lengo la kutambua upungufu wa virutubishi muhimu kwa mimea, wingi wa tindikali na chumvi kwenye udongo, aina za mbolea za kutumia na maeneo yasiyofaa kwa kilimo katika mkoa huo.
Kukamilika kwa mchakato huo Pwani, kunafikisha idadi ya mikoa iliyopimwa hadi sasa kufikia 19.
Upimaji wa afya ya udongo ukikamilika katika mikoa yote nchini, wizara inatarajia kuandaa ramani za kidijitali zitazokuwa na taarifa,sifa za udongo na aina ya mazao yanayofaa kulimwa.
Pia zitakuwa na aina za mbolea, zana za kilimo za kutumia na maeneo yasiofaa kwa kilimo, ili yabatishwe na kupangiwa matumizi mengine.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED