Madaktari, wauguzi matatani kifo mjamzito

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:21 AM Mar 31 2024
Daktari.
PICHA: MADAKTARI AFRIKA
Daktari.

MKUU wa Wilaya ya Tanga, James Kaji, amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Dk. Fedrick Sagamiko, kuwasimamisha kazi watumishi watano wakiwamo madaktari wawili kutoka Kituo cha Afya Mikanjuni, wanaotuhumiwa kusababisha kifo cha mjamzito, Fatma Suleiman (36).

Fatma ambaye ni mkazi wa Magaoni inadaiwa Machi 28, mwaka huu, alifanyiwa upasuaji na kuwekewa damu kinyume cha utaratibu, baada ya kwenda kituoni hapo kwa ajili ya kujifungua. Watumishi wengine ni wauguzi watatu. 

Amewataja wanaotakiwa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kuwa ni madaktari Hamisi Mohamed na Andrew Kidee na wauguzi watatu ambao ni Fadhia Hoza, Restituta Deusdedit na Muya Mhando. 

Kaji amesema baada ya vipimo vya awali ilibainika kwamba, mama huyo alikuwa akihitaji kufanyiwa upasuaji.

Amesema baada ya upasuaji huo mama na mtoto walikuwa kwenye hali nzuri, walipelekwa wodini kwa ajili ya uangalizi, huku wakisubiri kupewa ruhusa ya kurudi nyumbani.
 
 Amesema mama huyo akiwa wodini baadaye muuguzi aliyekuwa zamu alifika na kumwekea damu ambayo ilikuwa haiendani na kundi lake (damu iliyotakiwa kuwekwa kwa mgonjwa mwingine) jambo ambalo lilisababisha kifo chake.
 
 “Nimewaita kuzungumzia taarifa ya kifo cha Fatma Suleiman (36), mkazi wa Magaoni kilichotokea Machi 28, mwaka huu. “Fatma alikuwa ni mjamzito na alilazwa Kituo cha afya Mikanjuni Machi 28 mwaka huu saa 10 alfariji kwa tatizo la uchungu, aliendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na muuguzi,” amesema .

Amesema daktari wa zamu alipofika saa tisa mchana alionekana mama huyo mjamzito ana changamoto uchungu pingamizi na mtoto alikuwa ameanza kupata changamoto, hivyo madaktari waliamua kumfanyia upasuaji. 

Kwa mujibu wa Kaji, mgonjwa alifanyiwa upasuaji na kupata mtoto wa kike aliyekuwa na uzito wa kilo 3.4 na hakukuwa na changamoto yoyote kwa mama wala mtoto na katika wodi hiyo aliyolazwa kulikuwa na mgonjwa mwenye uhitaji wa kuwekewa damu na ilikuwa imeandaliwa na muuguzi aliyekuwa zamu. 

Kaji amesema muuguzi huyo alimwekea Fatma damu ambayo ilikuwa haihitajiki kwake bali kwa mgonjwa mwingine. “Niendelee kutoa rai kwa wauguzi na madaktari kuwa makini wakati wa utoaji wa huduma ili kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya kusababisha vifo,” ameonya. 

SABABU ZA KIFO 

Kaji amesema kifo hicho kimetokea kwa uzembe kwa kuwekewa damu ambayo hakuwa na uhitaji nayo na kupata mzio mkali (Allergic Reaction) na kumsababishia kifo.