Mbunge wa Lupembe mkoani Njombe, Edwin Swalle ametoa msaada wa mabati 80 kwa ajili ya kaya 11 zilizoathiriwa na mvua katika Kata ya Ikondo.
Pia, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe nayo imetoa msaada wa mabati 20, lengo likiwa ni kuwafariji waathirika hao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Februari 07, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Israel Mhada, amesema wamelazimika kutoa msaada huo kama sehemu ya kumuunga mkono mbunge.
Katibu wa Mbunge, Creiton Lulambo amesema kuwa mbunge ataendelea kusimama pamoja na wananchi katika nyakati zote, ikiwemo kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Mtendaji wa Kata ya Ikondo, Zakayo Matimbwi, amesema kuwa serikali ya kata iliwahifadhi waathirika katika maeneo salama, huku ikiendelea kuchangisha fedha ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida.
"Takribani kaya 11 zimeezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo. Baada ya kupata taarifa hizo, tulifika eneo la tukio na kupitia kaya moja baada ya nyingine ili kujiridhisha na kuona madhara yaliyosababishwa katika kaya hizo,” amesema Matimbwi.
Mmoja wa waathirika wa mvua hizo, Titus Kamonga amemshukuru mbunge kwa msaada wa mabati akisema kuwa yatasaidia kurejesha makazi yao baada ya nyumba zao kuharibika.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED