DRC, Tanzania zasaini mkataba kupewa hekta 60 kujenga bandari

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:42 PM Jun 09 2024
DRC, Tanzania zasaini mkataba  kupewa hekta 60 kujenga bandari
Picha: Mpigapicha Wetu
DRC, Tanzania zasaini mkataba kupewa hekta 60 kujenga bandari

SERIKALI ya Tanzania na DRC zimesaini mkataba wa kuimarisha Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza manufaa ya kijiografia na ushindani kwenye shoroba kwa ujumla.

Mkataba huo ni kwa DRC kuipatia Tanzania eneo la hekta 60 kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu nchini humo kwa lengo la kuongeza ufanisi. 

Mkataba huo ulisainiwa na Naibu Waziri Wa Uchukuzi Tanzania, David Kihenzile na Waziri anayeshughulikia masuala ya usafirishaji DRC, Marc Likombo, na kushuhudiwa na makatibu wakuu wa wizara hizo huku nchi ikiwakilishwa na Prof. Godius Kahyarara na Balozi wa Tanzania DRC, Said Mshana. 

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Godius Kahyarara alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa itawezesha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutoa huduma ndani ya DRC na kuondoa ulazima wa wateja kuja mara kwa mara bandarini. 

Alisema madereva wanaopeleka shehena DRC wataondokana na adha ya kusubiri kwa muda mrefu kwani mzigo ukifikishwa bandari kavu watakuwa na sehemu ya kukamilisha taratibu tofauti na hivi sasa ambapo kumekuwapo misongamano mingi barabarani wakisubiri ukamilishai wa nyaraka. 

Aidha, alisema sekta binafsi nchini yakiwemo mabenki, wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali watakuwa na fursa ya kufungua biashara zao katika bandari kavu hizi ikiwamo masoko maalum. Alisema bandari kavu hizo zitajengwa katika majimbo ya Katanga na Tanganyika. 

Kwa mujibu wa Profesa Kahyarara, DRC inaagiza zaidi ya asilimia 80 ya vyakula pamoja na asilimia 90 ya bidhaa za viwanda ikiwemo vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo nakadhalika. 

“Ninaona hii ni fursa kubwa ya kukuza uchumi wetu, uwepo wa Bandari Kavu utaongeza uhakika wa upatikanaji wa mzigo wa kutosha kupitia bandari ya Dar-es Salaam,”alisema. 

Aidha, alisema baada ya Bandari Kavu serikali kwa kushirikiana na ushoroba wa kati inaandaa mpango kabambe wa uwekezaji katika Ziwa Tanganyika kuwezesha Dar es Salaam kubaki kama lango kuu la nchi za ushoroba wa kati.   

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Naibu Waziri Wa Uchukuzi Tanzania, David Kihenzile alisema serikali imetenga jumla ya hekta 60 ambapo, hekta 15 za ardhi zimetengwa katika eneo la Bandari Kavu ya Katosho - Kigoma na hekta 45 katika eneo la Kwala- Pwani sambamba na kutoa hati miliki kwa ajili ya nchi ya DRC kujenga na kuendesha Bandari  Kavu. 

Naibu Waziri Kihenzile alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha usafirishaji na uchukuzi unarahisishwa hususani kwa mzigo mkubwa unaosafirishwa na DRC kupitia Bandari ya Dar es Salaam. 

Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa DRC, Likombo alisema kwa DRC imetenga hekta 15 katika eneo la Kasumbalesa na hekta 20 katika eneo la Kasenga-Jimbo la Haut Katanga; na hekta 25 katika eneo la Kasambondo- Kalemie Jimbo la Tanganyika sambamba na kutoa hati miliki kwa ajili ya Tanzania kujenga na kuendesha bandari kavu. 

Waziri Likombo aliongeza kuwa serikali ya DRC imefanya hivyo ili kurahishisha biashara baina ya nchi hizo mbili kwani DRC inaitegemea sana Nchi ya Tanzania katika kusafirisha mizigo yake. 

Mkataba huo unatajiwa kuongeza ufanisi na idadi ya mzigo unaosafirishwa katika myororo mzima wa uchukuzi, na kwamba takwimu zinazonyesha kwa 2022/23 tani milioni 3.5 za mzigo wa Kongo zilihudumiwa katika Bandari ya DRC.