‎Diwani aomba Mkuranga itangazwe Mji

By Yasmine Protace , Nipashe Jumapili
Published at 02:51 PM Feb 08 2026
Diwani wa Kata ya Msonga, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Msuko Msuko
Picha: Yasmin Protace
Diwani wa Kata ya Msonga, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Msuko Msuko

Diwani wa Kata ya Msonga, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Msuko Msuko, ameiomba Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuipandisha Halmashauri ya Mkuranga hadhi na kuitangaza rasmi kuwa mji, akitaja kasi kubwa ya maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika wilaya hiyo. ‎

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, diwani huyo amesema kuwa endapo Mkuranga itatangazwa kuwa mji, bajeti ya halmashauri itaongezeka kutoka takribani shilingi bilioni mbili hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni sita, jambo litakalosaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
 ‎
 ‎Amesema tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, wilaya ya Mkuranga imepata mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, miundombinu na huduma za kijamii.
 ‎
 ‎Akielezea maendeleo katika kata yake, Msonga, diwani Msuko Msuko amesema alipoingia madarakani mwaka 2020, Shule ya Sekondari Nasibu Ngani ilikuwa na mabweni mawili pekee na nyumba sita za walimu. Hata hivyo, kutokana na juhudi na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, shule hiyo kwa sasa ina mabweni 10 pamoja na nyumba 18 za walimu zilizojengwa kwa mfumo wa ‘two in one’, hali iliyoongeza idadi ya vyumba vya walimu kufikia 90.
 ‎
 ‎Aidha, amesema Serikali kupitia bajeti imeipatia kata hiyo zaidi ya shilingi bilioni 1.73 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu kutoka Mavunja kwenda Nasibu Ngani na Sotele, ambapo ujenzi unaendelea na mkandarasi yupo kazini.
 ‎
 ‎Katika hatua nyingine, diwani huyo amempongeza Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, kwa mchango wake mkubwa katika kuleta maendeleo wilayani humo, hususan katika kuboresha miundombinu ya barabara.
 ‎
 ‎Ameongeza kuwa licha ya bajeti za barabara kuonekana ndogo kila mwaka, lakini kutokana na mafungu makubwa ya fedha yanayotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia, kumekuwa na maboresho makubwa ya miundombinu hiyo.
 ‎
 ‎Kwa kumalizia, Msuko Msuko amempongeza Rais Samia kwa kuongeza fedha katika halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu, akisema hatua hiyo imechangia kuinua uchumi wa wananchi wa Mkuranga.