CHAUMMA wala ubwabwa kwa ushindi kiti kimoja uenyekiti mtaa

By Grace Mwakalinga , Nipashe Jumapili
Published at 01:04 PM Dec 01 2024
Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Mbeya, Ipyana Samson.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Mbeya, Ipyana Samson.

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kimefanya sherehe kwa kupika ubwawa baada ya mgombea wake, Brian Mwakalukwa, aliyekuwa akigombea nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Soko, Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuibuka mshindi.

Sherehe hiyo ilifanyika jana eneo la Soko la Mwanjelwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya chama hicho chini ya mwenyekiti wake, Hashim Rungwe, inayosema ‘Kupeleka ubwabwa shuleni na hospitalini’.

Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Mbeya, Ipyana Samson, alisema jana kuwa katika Mkoa wa Mbeya walisimamisha wagombea 130 kwa nafasi Uenyekiti wa Serikali za Mitaa, Vitongoji, Vijiji na wajumbe wa nafasi mchanganyiko na kundi la wanawake.

Alisema kati ya wagombea wote, Mwakalukwa ndiye aliyeibuka mshindi baada ya kuchaguliwa na wananchi kwa kura 42 akifuatiwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 38.

“Ni ushindi pekee wa chama chetu si tu kwa Mkoa wa Mbeya, bali nchi nzima. Hii ni ishara kuwa tunaaminiwa na wananchi kuibuka kidedea hasa katika eneo hili la mjini, tunajipanga kwa Uchaguzi Mkuu hapo mwakani  tutaongeza wanachama kutoka 300 wa sasa vilevile tutashimamisha wagombea kwenye nafasi za  udiwani na ubunge,” alisema Samson.

Alisema sherehe hiyo ya ubwawa imefanikishwa na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa, eneo ambalo mgombea wao ameshinda ambapo wametoa fedha kwa ajili ya kununua mchele na mahitaji mengine.

Aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ive Alex, alisema amefurahia mchakato wa uchaguzi ulivyokwenda hadi mgombea wa CHAUMMA kuibuka kidedea.

Alisema Mwakalukwa ni kiongozi aliyejaliwa hekima na busara na anatimiza majukumu yake kulingana na mahitaji ya wafanyabiashara.

Atupokile Eliachim, mkazi wa Mtaa wa Soko, mshindi wa nafasi ujumbe kwa tiketi ya CCM,  alisema amefurahishwa na ushindi wa Mwakalukwa na kuahidi kumpa ushirikiano mwenyekiti huyo, katika kutimiza majukumu yake.

Mwakalukwa alisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki na kuwaahidi wananchi kusimamia masuala ya usafi na uzoaji taka kuzunguka maeneo yote sokoni hapo ambapo ni moja ya changamoto kubwa.

Rungwe alijizolea umaarufu katika kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo alijinadi na sera ya ubwabwa, ambayo ilizua gumzo.