Bilioni 28/- zatumika soko jipya K’koo

By Pilly Kigome , Nipashe Jumapili
Published at 04:31 PM Feb 08 2026
Rais Samia Suluhu Hassan (kushoto)
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan (kushoto)

Zaidi ya Sh. bilioni 28 zimetumika kukarabati na kufanya maboresho Soko jipya la Kariakoo, fedha zilizotolewa na kuidhinishwa na Rais Samia Suluhu baada ya soko hilo kuungua mwaka Julai, 2021.

Fedha hizo zimeleta mageuzi makubwa katika soko hilo, ikiwamo kuweka mifumo ya kielektroniki, kuboresha mifumo ya miundombinu, mifumo rafiki ya wafanyabiashara.

Kadhalika, uwapo wa maji ya kutosha, magari ya zimamoto, maegesho ya magari, mifumo ya kifedha na huduma zingine za kijamii.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila,  ametoa maelekezo kwa wafanyabiashara ndogo wanaoendesha shughuli zao barabarani, kuziacha wazi barabara hizo kuanzia leo, ili kupisha soko jipya la kimataifa kuingilika kwa urahisi.

Chalamila amesema hawataweza kukubali kuona mfanyabiashara yoyote anaziba barabara za kuingia katika soko hilo la kimataifa, ambalo linategemewa ndani na nje ya nchi na fedha nyingi zimewekezwa hapo.

Aidha ametoa agizo kila mmoja awe mlinzi wa mwenziwe, ili kuweza kulinda hadhi ya soko hilo.