ZIC yakabidhi msaada wa vitabu vya mitaala sekondari

By Rahma Suleiman , Nipashe Jumapili
Published at 08:02 AM Jun 23 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Shirika la Bima Zanzibar ZIC likishirikina na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Fondation wamekabidhi msaada wa Vitabu vya Mitaala kwa Skuli za Secondari ili kukuza kiwango cha ufaulu katika Skuli za Mkoa ya Kusini Unguja.

SHIRIKA la Bima la Zanzibar (ZIC) limekabidhi msaada wa vitabu vya mitaala kwa shule za sekondari kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF).

Lengo la msaada huo ni kukuza kiwango cha ufaulu katika Shule za Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. Ulitolewa juzi makao makuu ya shirika hilo huko Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa ZIC, Jape Ussi alisema elimu ndiyo msingi wa maendeleo katika nchini na ni jukumu la kila mmoja kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuendeleza upatikanaji elimu bora kwa watoto.

“Katika kuendeleza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wetu ZIC tunaahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali katika kuona malengo ya viongozi wetu yanafanikiwa katika sekta ya elimu Zanzibar," alisema.

Alisema ni jukumu la kila mmoja kuona kuwa elimu inakuwa vizuri na wanafunzi wanafaulu katika mitihani yao ya taifa, ili kuwa viongozi wazuri wa baadaye.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema katika kusherekea miaka 55 ya shirika hilo, wameona fahari kushirikiana na Wizara ya Elimu kuwapatia vitabu vya mitaala kwa wanafunzi wa Zanzibar.

Alisema serikali inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha wanafunzi wote wa Zanzibar wanapata elimu iliyokuwa bora kulingana na mahitaji ya dunia yaliyopo hivi sasa.

Alisema kuwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora shirika hilo litaendelea kuunga mkono katika kutatua changamoto za kupata elimu kwa wanafunzi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), Sabra Mohamed alishukuru shirika hilo kwa kuchangia vitabu vya mitaala kwa ajili ya shule za sekondari katika Mkoa wa Kusini Unguja.

"Moja ya vipaumbele vyetu kama Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation ni kuhakikisha tunasaidia jitihada za kuimarisha upatikanaji elimu bora katika nchi yetu, ikiwamo kuweka miundombinu imara na endelevu kwa vijana wetu ili waweze kufikia malengo yao pamoja na malengo ya nchi yetu kwa ujumla," alisema.

Sabra alisema kupatikana msaada wa vitabu hivyo kunalenga kuondosha sifuri kwa wanafunzi wa Mkoa wa Kusini.

Hafla hiyo ya makabidhiano inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 55 ya Shirika la Bima la Zanzibar tangu kuanzishwa kwake Juni 20, 1969.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na watendaji kutoka ZIC.