Rehema: "Serikali, jamii iunge mkono bidhaa za mabinti waliohitimu mafunzo ya cherehani"

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 06:11 PM Jun 09 2024
Mkurugenzi wa Panda Initiatives, Rehema Sanga.
Picha: Halfani Chusi
Mkurugenzi wa Panda Initiatives, Rehema Sanga.

MKURUGENZI wa Taasisi ya Panda Initiatives, Rehema Sanga ameitaka serikali pamoja na jamii kununua bidhaa zinazozalishwa na mabinti 23 waliohitimu mafunzo ya ufundi cherehani kupitia mradi wa Wezesha Binti.

Rehema ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam, katika mahafali ya mabinti 23 waliohitimu mafunzo hayo yalioratibiwa na taasisi hiyo inayojihusisha na kuwawezesha, kuwainua vijana, wasichana, wanawake na makundi maalumu.

Amesema mradi huo wa Wezesha Binti unalenga kuboresha hali ya uchumi ya wasichana na wanawake vijana katika Kata ya Kivule kwa kuwapatia elimu mbalimbali ikiwamo za ujasirimali na ufundi.

Amesema mabinti hao watasaidia katika kukuza uchumi wa nchi na kwamba bidhaa watakazo zalisha zitaweza kuuzwa nje na ndani ya nchi hata kufikia soko la kimataifa.

“Tunaomba wafadhili wengine wajitokeze kuendelea kufadhili katika mradi huu, hatupokei ruzuku kutoka serikalini, hatuna vyanzo vingine vya fedha tunaomba misaada na ufadhili ili tuweze kuwakomboa vijana.

“Serikali iwaunge mkono kwa kununua bidhaa walizotengeneza wachangiwe katika kuanzisha kiwanda chao kidogo na kikundi chao cha Komboa Women Group tunafahamu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu itatusikia katika hili” amesema Rehema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Halamashauri ya Jiji la Ilala  

WAHITIMU  
Mhitimu wa mafunzo hayo Josephine Michael ameishukuru taasisi ya Panda Initiatives kwa kuwawezesha kupata mafunzo akibainisha kwamba yatawasaidia katika kupambana na umasikini.

“Nilichaguliwa katika mafunzo ya ushonaji baada ya kushindwa kumaliza kidato cha nne, nilifanya majaribio nikafaulu nikapata nafasi ya kufadhiliwa ninashukuru sana nimejifunza kushona nguo za aina zote, nisingekuja kusoma nisingejua kitu chochote kwa sasa hata kushona suti niko tayari ninatoa wito kwa mabinti wengine walioko mtaani wachangamkie fursa kama hizi zinapotokea" amesema

Mhitimu mwingine Masaa Warioba, amesema baada ya kumaliza kidato cha nne alipata taarifa kwa mjumbe wa serikali ya mtaa wake kuhusu taasisi hiyo kufadhili mabinti kupata mafunzo na kisha baada ya hapo akaamua kuchangamkia fursa.

“Ninashauri mabinti wenzangu wakisikia fursa ya ushonaji ni nzuri na inaweza kukubalishia maisha hata kulea familia kwa kuwa mafundi wengi huwa ninaona wana maisha mazuri” ameshauri