Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Ally Dau, amesema halmashauri hiyo inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 17.4 katika kipindi cha bajeti ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Dau aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani pamoja na kikao cha pili kilichojadili malengo ya ukusanyaji na matumizi ya bajeti hiyo.
Amesema kati ya fedha zinazotarajiwa kukusanywa, kiasi cha shilingi bilioni 8.9 kitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, barabara na maeneo mengine ya kijamii na kiuchumi.
“Malengo ya halmashauri yetu ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 17 katika mwaka wa fedha 2026/2027, fedha ambazo zitasaidia kufungua na kuimarisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo,” amesema Dau.

Ameongeza kuwa Halmashauri ya Mkuranga kwa sasa imeingia katika mpango wa maendeleo, hivyo imeendelea kuwakaribisha wawekezaji kufuata taratibu rasmi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amempongeza Samia Suluhu Hassan, kwa kuiongezea halmashauri fedha katika bajeti, hatua iliyowezesha kununuliwa kwa zaidi ya madawati 400 ambayo yamesambazwa katika shule za msingi na sekondari za serikali.
Amesema ugawaji wa madawati hayo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi kwa kuwaondoa katika kukaa chini, hivyo kufanya shule kuwa za kisasa na rafiki kwa elimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wilaya ya Mkuranga, Waziri Kondo, amesema vikao hivyo vya Baraza la Madiwani vililenga kujadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya mwaka pamoja na masuala ya matumizi ya bajeti.
Aidha, amewatoa wasiwasi madiwani kuhusu maandalizi ya halmashauri kukabiliana na ongezeko la wanafunzi ifikapo mwaka 2028, akisisitiza kuwa tayari halmashauri imejipanga kwa kuandaa idadi kubwa ya madawati ili kukidhi mahitaji yatakayojitokeza.

Akizungumzia mpango wa “Master Plan” unaotekelezwa wilayani humo, Kondo amesema mpango huo utasaidia Mkuranga kuwa na mpangilio mzuri wa makazi na maendeleo, hivyo kuwataka wananchi na wanunuzi wa viwanja kufuata taratibu rasmi kupitia ofisi za halmashauri kabla ya kuanza ujenzi.
Naye Afisa Mipango wa Wilaya ya Mkuranga, Idrisa Jukulu, amesema ununuzi holela wa viwanja umekuwa changamoto kubwa kwani unainyima halmashauri mapato yanayostahili kukusanywa.
Amesema halmashauri imepokea ombi kutoka kampuni ya ZEDEM inayomiliki ardhi katika kata za Mbezi, Shungubweni na Dondo kwa lengo la kupima, kupanga na kutambua maeneo hayo ili yaweze kutumika kwa tija, hususan katika maendeleo ya sekta ya viwanda.
“Kwa kuzingatia uhalisia, sekta ya viwanda inakua kwa kasi katika eneo lote la Mkuranga, hivyo mpango huu utaongeza thamani ya ardhi, halmashauri itanufaika kwa kupata maeneo ya umma na pia kupunguza migogoro ya ardhi inayosababishwa na kutokupimwa,” amesema Jukulu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED