Miradi ya nishati kunufaisha wananchi wanaoizunguka

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:30 AM Sep 01 2024
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo yana miradi mikubwa ya nishati watanufaika na miradi hiyo kupitia upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Kapinga amesema hayo  Agosti 30, 2024 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Ally Kasinge Mbunge wa Kilwa Kusini ambaye alitaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuhakikisha Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi ambako kuna visima vya Gesi Asilia na mitambo ya kuchakata gesi  kinapata umeme wa uhakika.

"Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa  Nishati, Dkt. Doto Biteko alishatoa maelekezo kuhakikisha wananchi hawa sio tu wanapata umeme wa uhakika bali na huduma nyingine za kijamii ziweze kuimarishwa." alisema Kapinga 

Amelihakikishia Bunge kuwa, tayari Serikali imeanza kulifanyia kazi  agizo hilo  kwa kuhakikisha wananchi wa Songosongo wanapata umeme wa uhakika na huduma nyingine za kijamii ambazo zinaendana na miradi iliyopo katika maeneo yao.

Akizungumzia upelekaji umeme wa gridi kwenye maeneo ya Visiwa, Kapinga amesema Tanzania ina visiwa takriban 120 na Serikali imeanza kufanya tathmini ya kufikisha umeme wa gridi katika maeneo hayo.

Ameongeza kuwa, kwa sasa visiwa hivyo vinatumia umeme wa jua ambapo Serika imeweka ruzuku ya asilimia 50 hadi 55 ili wananchi wapate umeme wa uhakika kwa muda wote.