Yanga yaanika rasmi malengo matatu CAF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:49 PM Jun 21 2024
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamesema malengo yao kuelekea msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2024/2025 ni kufika hatua ya nusu fainali, fainali au kubeba taji la Afrika, imeelezwa.

Msimu uliopita Yanga ilitolewa katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema jeuri ya kuzungumza matarajio hayo wanaipata kutokana na kikosi kilichopo, na kile ambacho watakiongeza kuelekea msimu ujao.

Kamwe alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kubakisha wachezaji tegemeo, hivyo kikosi kitakuwa na makali zaidi kwa sababu kitaundwa na nyota wale wale lakini watakiboresha kwa kuongeza wengine ambao wana viwango vikubwa zaidi na kuifanya timu hiyo kuwa tishio.

"Kwanza tumefanikiwa kumbakisha Kocha Miguel Gamondi, hiyo peke yake ni jambo kubwa sana, lakini tumewabakisha wachezaji wetu tegemeo ambao walituheshimisha msimu uliopita, kama vile haitoshi tunaongeza na mashine nyingine.

Nimechungulia mimi majina ya wachezaji wapya, ni hatari, yaani msimu ujao mbali na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA, tuna malengo mengine matatu, kwanza kabisa ni akili yetu ni kutwaa ubingwa wa Afrika, kama tukishindwa basi tufike fainali tu, na kama ikishindikana tuishie nusu fainali," alisema Kamwe.

Aliongeza hatua hizo tatu itakuwa ni heshima kubwa kwa Yanga kwa sababu haijawahi kufikia hatua hiyo tangu mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), yalipoanzishwa.

"Tulikuwa hatujaingia hatua ya makundi kwa miaka 24 hivi, tukaingia na msimu huo huo tukafika robo fainali ambayo tulikuwa hatujawahi kufika tangu mfumo huu wa makundi uanze, na huu ulikuwa msimu mmoja tu, sasa msimu wa pili tunahitaji tuvunje rekodi yetu wenyewe, tukifika nusu fainali tu tutakuwa tayari tumeshafanya hivyo.

Chochote kikitokea baada ya hapo ni mafanikio, lakini bado ikitokea tukienda fainali ni moja ya malengo tuliyojiwekea na kuchukua ubingwa pia ikiwezekana, hilo kwetu linawezekana kutokana na kikosi tutakachokijenga msimu ujao," Kamwe alisema.

Wakati huo huo, Mabosi wa Yanga wamesema wamemwongeza mkataba wa mwaka mmoja kiungo mkabaji, Zawadi Mauya.

Kamwe alisema Mauya ataendelea kusalia ndani ya kikosi hicho kutokana na mchango wake bado unahitajika.

Hata hivyo taarifa kutoka Yanga zinasema Mauya amepewa mkataba mpya kutokana na klabu hiyo kumkosa, Yusuph Kagoma aliyekuwa anaitumikia Singida Black Stars, kudaiwa tayari ameshamalizana na watani zao, Simba.

Chanzo chetu kinasemea klabu hiyo pia inajipanga kuwaongeza mikataba wachezaji wake, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Jonas Mkude, Kibwana Shomari na nahodha, Bakari Mwamnyeto ili waendelee kukipiga katika kikosi hicho kilichotwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara 30.

"Yanga haitaki kupoteza wachezaji wengi ambao iliwasaidia kufika ilipofika, itawabakisha wale nyota, halafu inatarajia kuwapa mikataba wale ambao walikuwa hata hawachezi mechi nyingi kwa sababu imeonekana hata wakiingia wanatekeleza kile ambacho mwalimu anakitaka, mfano mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns  ilipowakosa wachezaji wake nyota," kiliongeza chanzo chetu.

Yanga itatajwa pia iko mbioni kukamilisha mazungumo ya kumnasa beki wa kushoto wa FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Chadrack Boka, ili kuchukua nafasi itakayoachwa na Joyce Lomalisa, aliyemaliza mkataba wake huku  Mkongomani mwingine, Emmanuel Lobota, anayecheza nafasi ya winga, kutoka Singida Black Stars na Agee Basiala, kiungo wa DR Congo, anayekipiga kwenye Maniema Union huenda wakatua Jangwani.