Sinema yakolea Simba SC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:20 AM Jun 13 2024
Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji 'Mo Dewji'.

WAKATI Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji 'Mo Dewji' amerejea katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na kusema amekuja na mikakati sita itayoiwezesha timu yao kuimarika, Salim Abdallah 'Try Again' naye amerudi ndani ya uongozi wa klabu hiyo, muda mchache baada ya kutangaza kujiuzulu.

Akizungumza muda mchache baada ya Try Again kujiuzulu, Mo Dewji, alisema amerejea na nguvu mpya na atahakikisha kikosi cha Simba kinarejea katika ubora wake kama ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita.

Mo alisema kufanya vibaya kwa Simba katika misimu miwili iliyopita kumetokana na usajili mbovu wa wachezaji pamoja na kuwa na benchi la ufundi lisilokuwa na viwango.

Mfanyabiashara huyo amewahakikishia wanachama na mashabiki wa Simba ataendelea kuwa mwekezaji na hatatoka leo wala kesho kama baadhi ya watu wanavyodhani kwa sababu uwepo wake ndani ya klabu hiyo 'unabebwa' zaidi na ushabiki, wala si uwekezaji au ufadhili.

Alisema kilichoifelisha Simba msimu huu ni kushindwa kutengeneza timu ya ushindani na hiyo ilitokana na kusajili idadi kubwa ya wachezaji wenye viwango vya chini ambavyo hakikufanana na hadhi ya klabu hiyo.

"Kwanza kabisa hatukuwa na umoja, hasa baada ya uchaguzi, malumbano na mgawanyiko umeendelea kututafuna, jambo hili halina afya, niwaombe tumalize tofauti zetu za uchaguzi na kuzikika kabisa.

Pili, tumeshindwa kutengeneza timu bora ya ushindani, eneo la benchi la ufundi halikuwa zuri, imesababisha hata kupoteza falsafa yetu ya pira-biriani, hili ni eneo muhimu la kufanyia kazi, naahidi tutashirikiana na wenzangu kusuka upya eneo hilo na tatu. 

Tumeshindwa kukidhi kiu ya Wana-Simba katika usajili, nyota wengi waliosajiliwa viwango vyao havikuwa bora, kwa hiyo ningependa kuwaahidi, nitashirikiana na viongozi wenzangu, pamoja na wataalamu kufanya usajili bora, katika ukubwa utakaokidhi matamanio ya wanachama na mashabiki," alisema Mo.

Aliutaja mkakati wake wa nne ni kushirikiana kwa karibu na wanachama, mashabiki na viongozi wenzake kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ndani ya klabu hiyo, ili watu waanze kupata hisa za umiliki.

"Lingine ni eneo la ukuaji wa wanachama na wapenzi, nitashirikiana na viongozi wenzangu ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ili Wana- Simba wapate hisa zao stahiki na kuwa wamiliki kamili wa klabu, hili ni muhimu katika ukuaji wa klabu, tano ni miundombinu ya klabu iliyopo Bunju haikidhi haja, hivyo ni lazima tulifanyie uwekezaji ulio bora kufanana na hadhi ya Simba. 

Mkakati wa sita, Simba inahitaji kuwa na mchakato wa kuibua vipaji, tutalifanyia kazi zaidi," aliahidi bilionea huyo na hapo hapo alitangaza kumteua Try Again kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

Pia amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuimarisha umoja wao kwa sababu hakuna muda tena wa kulalamika, kupiga kelele na kupakana matope, bali wanatakiwa kuijenga Simba mpya.

"Nimemwomba Salim (Try Again), kubaki kwenye bodi kwa niaba ya mwekezaji na amekubali, na hivi karibuni nitateua wajumbe wengine ili bodi iwe kamili kuanza kazi. Narejea nikiwa na nguvu na ari mpya, maarifa ya kurejea Simba ninayoitaka, naongozwa zaidi na ushabiki, wala siyo ufadhili na uwekezaji, sitoiacha Simba leo wala kesho," alisisitiza.

Mo alitangaza kujiuluzu nafasi yake Septemba, mwaka 2021 na kumteua Tyr Again, ambaye kipindi hicho alikuwa ni makamu wake kuongoza jahazi hilo la Wekundu wa Msimbazi.

"Kuna baadhi ya wachezaji siyo waaminifu, hawajitumi na kuitendea haki klabu yetu, viongozi wanaokuja wanapaswa kuwachukulia hatua kali ambazo zitafanya kila mchezaji kuwajibika. Tunasajili wachezaji kwa pesa nyingi, tunalipa mishahara lakini si waaminifu, niseme tu, nitaongea na uongozi mpya ili kuwachukulia hatua hawa ambao si waaminifu," alisema Try Again wakati anatangaza kujiuzulu.