Simba yavujisha usajili, Kramo yumo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:28 AM Jun 25 2024
Aubin Kramo.
Picha: Mtandao
Aubin Kramo.

ZILE tetesi za usajili za Klabu ya Simba kupata saini za baadhi ya wachezaji akiwamo Elie Mpanzu kutoka Klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Yusuph Kagoma wa Singida Black Stars, zinaelekea kukamilika baada ya Meneja Habari na Mawasiliano wa miamba hiyo, Ahmed Ally, kugusia usajili wao, huku akitangaza rasmi kuwa winga wa klabu hiyo aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu, Aubin Kramo, amepona na yupo tayari kwa msimu mpya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ahmed alisema Mpanzu na Kagoma ni wachezaji wazuri wenye hadhi ya kuichezea Klabu ya Simba, huku akiwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa na subira kwani siku si nyingi wataweka wazi majina ya wachezaji wote waliosajiliwa pamoja na benchi la ufundi.

"Mpanzu, ni mchezaji mzuri mwenye hadhi ya kucheza klabu kubwa kama Simba, anakuja au haji ni jambo la kusubiri, hivi karibuni tu kila kitu kitafahamika," alisema Ahmed.

Winga huyo wa kulia ni mmoja wa wachezaji wanaotajwa kuwa watatua Msimbazi kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho ambacho ni kama kinaanza kujengwa upya baada ya anguko kuu msimu uliomalizika.

Akimzungumzia Kagoma, alisema huu ndiyo muda wake sahihi wa kwenda kwenye klabu hiyo.

"Kagoma, kiungo mkabaji wa maana sana, ana kipaji kikubwa,  kwa sasa ni mchezaji wa Singida Black Stars, tusubiri kwanza, eneo letu la kiungo mkabaji lina mashaka sana kwa siku za hivi karibuni, kama anatua naamini kwa ubora aliyokuwa nao, atatusaidia sana, ni muda wake sahihi wa kuja Unyamani," alisema Meneja habari huyo ikionyesha tetesi hizo zinaelekea kukamilika.

Awali, ilitajwa kuwa mchezaji huyo angetua Klabu ya Yanga, lakini ghafla kibao kiligeuka na Simba ikafanya naye maongezi ambayo yanaelezwa kufanikiwa.

Alipuuzia tetesi za kuondoka kwa beki Fondoh Che Malone, ikitajwa kuwa amepata ofa kwenye Klabu ya Kasimpasa FC ya Uturuki.

"Che Malone haendi popote, bado ni mchezaji wa Simba, ana mkataba na hatuwezi kumruhusu kuondoka kwa sababu tuna mipango naye," alisema.

Klabu ya Simba pia imetangaza rasmi urejeo wa winga wake iliyomsajili mwanzoni mwa msimu uliopita, lakini haikumtumia kutokana na majeraha ya muda mrefu, Kramo.

Winga huyo na kiungo mshambuliaji alisajiliwa kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast, alicheza mechi tamasha la Simba Day kati ya timu yake na Power Dynamos, Agosti 6, mwaka jana akiingia kutokea benchi, lakini baada ya hapo aliandamwa na majeraha yaliyowalazimu mabosi wa klabu hiyo kukata jina lake kwenye orodha ya wachezaji wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwekwa mwingine wa kigeni, huku akiendelea kupata mshahara na stahiki zake kama kawaida.

"Kramo alikuwa majeruhi karibuni msimu mzima, tumemtibu mwanzo hadi mwisho, huku tukimlipa stahiki zake zote hili inafaa tujipongeze, kwa sasa kijana amepona kabisa, tutakapokwenda kuweka kambi nchini Misri mwanzoni mwa mwezi wa saba atakuwa sehemu ya wachezaji wataokwenda kambini kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao. Muda wa Wanasimba kumtazama na kumfaidi Kramo sasa umefika," alisema Ahmed.